Timu
ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) itacheza mechi ya kirafiki na
Burundi (Intamba Mu Rugamba) Aprili 26 mwaka huu ikiwa ni sehemu ya
maadhimisho ya miaka 50 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Taifa
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager tayari ipo kambini
Tukuyu mkoani Mbeya ikijiandaa kwa ajili ya mechi hiyo ikiwa na
wachezaji waliopatikana katika programu maalumu ya kusaka vipaji.
Baadaye
wachezaji wengine wa Taifa Stars ambao wapo nje ya programu ya kusaka
vipaji wataungana na wenzao kabla ya kutengeneza kikosi cha mwisho
kitakachoivaa Burundi.
Mechi
hiyo itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam itachezeshwa na
waamuzi wanaotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu
(FIFA) kutoka nchini Kenya.
TIMU YA WATOTO WA MITAANI YACHACHAFYA BRAZIL
Timu
ya Watoto wa Mitaani ya Tanzania imefanikiwa kuingia nusu fainali ya
mashindano ya Kombe la Dunia yanayofanyika Rio de Janeiro nchini Brazil
baada ya jana kuifunga Indonesia kwa jumla ya mabao 5-3.
Hadi
muda wa kawaida wa mchezo huo unamalizika timu hizo zilikuwa
zimefungana mabao 2-2 ndipo ikatumia mikwaju ya penalti kuamua mshindi.
Tanzania ilipata penalti tatu dhidi ya moja ya wapinzani wao.
Kwa
matokeo hayo, Tanzania sasa itacheza mechi ya nusu fainali leo dhidi ya
Marekani ili kupata timu zitakazocheza mechi za fainali na kutafuta
mshindi wa tatu. Mechi za fainali na kutafuta mshindi wa tatu zitachezwa
kesho (Aprili 6 mwaka huu).
Timu nyingine zilizoingia nusu fainali na mechi zake zinachezwa leo (Aprili 5 mwaka huu) ni Burundi itakayocheza na Pakistan.
Katika
mechi zilizopita, Tanzania ilitoka sare ya mabao 2-2 na Burundi,
ikaitandika Argentina mabao 3-0 ikailaza Nicaragua mabao 2-0 na
ikafungwa na Philippines mabao 2-0.
No comments:
Post a Comment