tuwasiliane

Sunday, April 6, 2014

RUVU SHOOTING YASIMAMISHA WACHEZAJI WATATU


UONGOZI wa timu ya Ruvu Shooting umewasimamisha kwa muda wachezaji wake watatu ambao waliondoka kambini asubuhi juzi, Ijumaa bila kuaga na kuelekea kusikojulikana.
Wachezaji hao ni Juma Seif (Kijiko), Ibrahim Suzan (Chogo) na Cosmas Ader ambao kwa pamoja walitoroka kambini huku wakijua timu ipo katika maandalizi ya mchezo mgumu na muhimu dhidi ya Azam ya Dar es salaam utakaochezwa siku ya Jumatano katika uwanja wa mabatini.

Msemaji wa Ruvu Shooting Masau Bwire alisema kwamba, uongozi wa timu yake chini ya mwenyekiti wake Kanali Charles Mbuge haukufurahishwa na kitendo cha wachezaji hao kutoroka kambini, hivyo kuamua kuwasimamisha na kuwazuia kufika kambini mpaka mechi dhidi ya Azam itakapomalizika.

Bwire alisema, wachezaji hao watatakiwa kuripoti kambini mara baada ya mchezo wa Azam ambapo watatakiwa kujieleza kwa maandishi kwa nini walitoroka kambini, walikokuwa na walichokuwa wakikifanya huko.
"Tunalazimika kuchukua taadhali kubwa kuelekea mchezo wa Jumatano dhidi ya Azam, vitendo vya utovu wa nidhamu kama vilivyooneshwa na wachezaji hao hatuwezi kuvifumbia macho, lazima tuchukue hatua za haraka kwani, vinaweza kutuletea matokeo mabaya tofauti na matarajio yetu" alisema Bwire.

Alisema timu yake imedhamilia kuonesha maajabu makubwa katika mchezo huo kwa kuibuka na ushindi na kuwa timu ya kwanza na pengine pekee msimu huu kuifunga timu ya Azam.

Aidha Bwire alisema kwamba, endapo itabainika kuwepo kwa mchezaji yeyote kambini kuonesha kitendo chochote cha utovu wa nidhamu kinachoweza kuvuruga maandalizi dhidi ya mchezo na Azam, uongozi hautasita kumchukulia hatua kali za kinidhamu, lengo ni kuhakikisha umoja wa timu unaimarika ili kupata ushindi katika mchezo huo.

No comments:

Post a Comment