tuwasiliane

Wednesday, August 14, 2013

MSHAMBULIAJI MPYA WA SIMBA BETRAM MWOMBEKI AWEKEWA PINGAMIZI NA PAMBA YA MWANZA

 
Mshambuliaji aliyetokea kukonga mioyo ya mashabiki wa Simba kwa kufumania nyavu, Betram Mwombeki amekwaa kisiki katika usajili wake kuichezea timu hiyo baada ya kuwekewa pingamizi na klabu yake aliyoichezea msimu uliopita, Pamba ya Mwanza.
Awali iliripotiwa kuwa Mwombeki amesajiliwa na timu hiyo akitokea nchini Marekani, hata hivyo Pamba wamepinga taarifa hizo na kusema kuwa mchezaji huyo aliichezea timu yao Ligi Daraja la Kwanza na kufunga mabao mawili msimu uliopita.
 
Mwenyekiti wa Pamba, Kazimoto Miraj Muzo aliiambia Mwananchi kuwa Mwombeki alikuwa Marekani miaka ya nyuma na mwaka jana alijiunga na Pamba wakati wa dirisha dogo la usajili na kucheza mechi kadhaa tofauti na taarifa kuwa ametokea Marekani.
 
Muzo alisema kuwa hakuweza kucheza mechi nyingi kutokana na kukabiliwa na maumivu ya goti. “Si kweli kuwa ametokea Marekani, tupo hapa na aliichezea timu yetu. Tuliwaambia Simba, wakabisha na sasa tutakutana mbele ya sheria,” alisema Muzo.
 
Alifafanua kuwa walizungumza na Makamu Mwenyekiti wa Simba, Joseph Itang’are kuhusiana na usajili wa mchezaji huyo, lakini hakuonyesha kujali taarifa hiyo.
“Tumewasilisha vielelezo vyetu TFF, tunasubiri matokeo ya kikao cha Kamati ya Alex Mgongolwa kutoa uamuzi wake, tumedhamiria kupigania haki yetu mpaka mwisho” alisema.
 
Alisema kuwa kiasi gani cha fedha watakachoidai Simba iwalipe ni siri, kwani daima wao huwa hawapendi kuweka hadharani masuala ya fedha, hasa za kumuuza mchezaji.
Itang’are alipoulizwa kuhusiana na sakata hilo alithibitisha kuongea na Pamba na kuahidi kulifanyia kazi. “Pamba ni ndugu zetu, miaka ya nyuma walitupa wachezaji wengi kama Hussein Marsha, John Makelele, George Masatu, Juma Amir na wengine, na kwa hili sidhani kama tutashindwana,” alisema Itang’are.
 
Wakati Simba inakabliwa na kikwazo kuhusiana na Mwombeki, Yanga inaelekea kupeta kwa mchezaji, Mrisho Ngassa kutokana na ukweli kuwa Simba hajawasilisha taarifa nyingine zaidi ya mkataba tu.
SOURCE: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment