
TAIFA STARS inacheza mechi ya pili ya mchujo ya Kombe la Dunia ugenini leo Jumamosi dhidi ya wenyeji Morocco ‘Lions of the Atlas’ huku ikipania kupata matokeo mazuri.
Mechi hiyo ya nne kwa Taifa Stars katika michuano
hiyo hatua ya makundi inachezwa saa 3:00 usiku kwa saa za hapa, ambapo
kwa Tanzania itakuwa saa 5:00 usiku kwenye Uwanja wa Grand Stade, mjini
Marrakech.
Akizungumzia mechi hiyo, Kocha wa Stars, Kim
Poulsen amesema timu yake inatarajia kucheza vizuri lengo likiwa ni
kuhakikisha inapata matokeo baada ya dakika 90 za mechi hiyo
itakayochezeshwa na Daniel Frazier Bennett kutoka Afrika Kusini.
“Unapocheza ugenini ni lazima uwe makini na
mwangalifu. Usiruhusu mpinzani wako akakuvuruga hasa dakika 20 za
mwanzo. Lengo letu kuja hapa ni kufanya vizuri, na tumejiandaa kimwili
na kiakili,” alisema Kim ambaye ameiongoza Stars kushinda mechi mbili
nyumbani dhidi ya Gambia na Morocco na kupoteza ugenini mbele ya Ivory
Coast katika Kundi hilo la C.
Ubora wa Stars katika mechi hiyo ni katika
kumiliki mpira na kutoa pasi zitakazowafanya kushambulia kwa urahisi
wakati Morocco inategemea zaidi uwezo wa mchezaji mmoja mmoja na wengi
wao wa kikosi cha kwanza wanacheza mpira wa kulipwa Ulaya.
Kwa upande wa maandalizi, Kim alisema Stars
inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imejiandaa vizuri kwani
ilikuwa na kambi ya wiki moja nyumbani, wiki moja nyingine ikapiga kambi
nchini Ethiopia, na baadaye hapa Marrakech ambapo pia imekuwepo kwa
wiki nzima ikijiwinda kwa mechi hiyo.
Ikiwa nchini Ethiopia ilicheza mechi ya kirafiki
dhidi ya Sudan iliyomalizika kwa timu hizo kutoka suluhu huku Kim
akiwapa fursa ya kucheza wachezaji 16 akiwemo Haruni Chanongo aliyecheza
dakika kumi za mwisho, ikiwa mechi yake ya kwanza baada ya kuitwa
katika kikosi hicho kwa mara ya kwanza.
Ndani ya miaka miwili, Stars itakuwa inakutana na
Morocco kwa mara ya nne. Mwaka 2011 katika mechi za kutafuta tiketi ya
Fainali za Kombe la Afrika mwaka 2012 nchini Afrika Kusini, Stars
ilifungwa nje ndani (1-0 jijini Dar es Salaam na 3-1 jijini Marrakech).
Lakini katika mechi iliyopita Machi 24 mwaka huu
Stars iliibuka na ushindi wa mabao 3-1, yote yalifungwa kipindi cha
pili. Shukrani kwa mabao hayo ya Mbwana Samata (mawili) na Thomas
Ulimwengu.
Kim alisisitiza kuwa malengo yake kwa sasa ni
kupigania nafasi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia na kwamba timu
yake imekuwa ikifanya vizuri kadri inavyoendelea kucheza ikiwa
imeshafunga mabao matano katika mechi hizo za mchujo.
“Tulianza safari kwa kufungwa 2-0 ugenini na Ivory
Coast. Katika mechi ile hatukupata bao na tukamaliza tukiwa kumi
uwanjani baada ya mchezaji wetu mmoja kutolewa kwa kadi nyekundu. Lakini
kadri tunavyoendelea katika mashindano ndivyo timu inavyozidi
kuimarika.
“Mechi hizi za Kombe la Dunia unatakiwa kushinda
nyumbani zote, mipango ambayo kwetu bado inakwenda vizuri. Tukiwafunga
Morocco kwao tutazidi kuimarika. Tunajua mechi itakuwa ngumu, nasi
tumejipanga kwa hilo tukijua Morocco wanacheza nyumbani na watakuwa
katika shinikizo kubwa kutoka kwa mashabiki wao,” alisema Kim aliyeanza
kuinoa Stars tangu Mei mwaka jana.
Atachezesha washambuliaji wangapi mwisho? Jibu la Kim katika
swali hilo ni kuwa timu iko kwa ajili ya kutengeneza nafasi za kufunga,
hivyo washambuliaji inabaki kuwa suala la namba tu.
Lakini akaongeza kuwa aina yao ya kushambulia itategemea na staili ya uchezaji ya wapinzani wao.
Kwa hapa Marrakech mechi hiyo imekuwa haizungumzwi
mara kwa mara, na kubwa ni kuwa Wamorocco wengi wanaamini kuwa timu yao
ambayo hadi sasa ina pointi mbili haina nafasi ya kusonga mbele katika
hatua inayofuata ya michuano hiyo. Kikosi kinachotarajia kuanza cha
Stars huenda kikapangwa hivi; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Shomari
Kapombe, Aggrey Morris, Kelvin Yondani, Frank Domayo, Mrisho Ngasa,
Salum Abubakar, Thomas Ulimwengu, Amri Kiemba na Mbwana Samata.
No comments:
Post a Comment