Kwa mujibu wa naibu katibu mkuu wa CUF bara bwana Julius Mtatiro kuwa
Mhe.
Katani alipigiwa simu leo mchana na kutakiwa kuripoti CENTRAL POLICE.
Alisindikizwa na baadhi ya viongozi na mwanasheria. Walipofika aliwekwa
chini ya Ulinzi na akajulishwa kuwa angesafirishwa leo hii kupelekwa
Mtwara ambako anapaswa kujibu tuhuma zinazomkabili.
Yeye(Mtatiro)na
Mwenyekiti Taifa (Prof. Lipumba) tumekwenda MAKAO MAKUU YA JESHI LA
POLISI na kukafanya kikao kifupi na IGP Mwema na DCI Manumba juu ya
masuala hayo. Tumekubaliana kuwa atasindikizwa na makachero kesho
asubuhi kuelekea Mtwara kwa ndege na kisha taratibu za kisheria
zitaendelea hukohuko.
Wanasheria na mawakili wetu na viongozi
pia watakuwa Mtwara kujua suala hili litakwendaa vipi. Kabla Mhe. Katani
hajakamatwa leo, amewahi kuhojiwa mara kadhaa na makachero wa polisi
Mtwara na DSM kabla kabisa ya vurugu za hivi majuzi na mara zote
alionesha ushirikiano mkubwa.
Tumejulishwa kuwa kati ya watu
wanaoweza kukamatwa baada ya Mhe. Katani ni pamoja na Mhe. Selemani
Bungara(MB) - Kilwa Kaskazini pamoja na viongozi kadhaa waandamizi.
Tumewajulisha viongozi wetu wasiwe na hofu, wasiondoke makwao na
ikiwezekana wajipeleke polisi wakijua wanatafutwa.
Cha
kushangaza ni kuwa, viongozi hawa wote wanaokamatwa, mara kadhaa
wamewahi kuendesha mikutano mikubwa na halali iliyolindwa na polisi
ambapo walipinga mpango wa serikali kusafirisha gesi kwenda DSM bila
kuhakikisha maslahi ya Mikoa ambayo gesi imevumbuliwa. Na haya
waliyafanya kwa kujenga hoja za kawaida kabisa majukwaani, zaidi ya hapo
hawajawahi kuhusika na masuala ya uchochezi.
Tumemweleza IGP
na DCI kuwa wawaambie serikali kuwa wao serikali ndo wamechochea vurugu
za Mtwara kwani JK mwenyewe aliwaahidi wananchi wa Mtwara masuala kadhaa
kuhusu gesi na hadi leo hayajatekelezwa. Tumewaeleza waziwazi kuwa
suala la gesi siyo jepesi sana na halitamalizwa kwa kuwakamata wanasiasa
wasio na hatia.
Suala la gesi litamalizika kwa salama ikiwa
serikali itafungua milango ya mazungumzo na maelewano na wananchi
inakotolewa ikiwa ni pamoja na juhudi kubwa za kuwaelimisha wananchi wa
mikoa husika na kuwatengenezea miradi mingi yenye tija ambayo italeta
ajira na kupanua uchumi wa wananchi wa mikoa ya kusini ili waondokane na
umasikini wa kutupwa.
Serikali iache kiburi ambacho hakina
mantiki kwa sasa, ifanye kazi kubwa ya kulitatua suala hili kwa busara.
Kuwakamata viongozi wetu siyo suluhisho, tutaendelea kutoa maoni na
mapendekezo yetu kama chama bila kificho chochote hata kama watatukamata
wote. Serikali itatue kiini cha tatizo, iache kutibu matokeo.
Mwisho wa siku ukweli utasimama, Wananchi wa Lindi na Mtwara wasikilizwe na tuache ubabe usio na maana.
Ndiyo, gesi ilinufaishe taifa, lakini tuwe na utaratibu maalum, tuwe na
sera ya gesi na ikiwezekana tuboreshe sheria zetu ili kufanya
rasilimali za taifa zilinufaishe taifa pamoja na wakazi wa maeneo ambako
rasilimali imepatikana.
No comments:
Post a Comment