Takriban watu 30 wanashikiliwa na jeshi la Polisi mkoani Iringa, kufuatia vurugu zilizozuka mapema asubuhi ya leo zikiwahusisha wafanyibiashara ndogondogo maarufu kama wamachinga na askari hao.
Vurugu hizo, ambazo zimeelezwa kuwa na msukumo wa kisiasa zaidi, zimehusisha wamachinga ambao walikuwa wakitaka kufanya biashara zao katika eneo maarufu la Mashine tatu, huku eneo hilo likiwa lilishakatazwa kutumika kwa shughuli hiyo.
Hadi tunaenda mtamboni, hakukuwa na taarifa zozote za kuuawa kwa mtu yeyote ingawa majeruhi kadhaa walikuwa wanaelezwa kuwa walikuwa wamepelekwa hospitali kupatiwa matibabu.
CHANZO CHA VURUGU:
Vurugu za leo, zimetokana na mvutano wa muda mrefu sasa ambao kwa namna moja umeelezwa kuwa umekuwa ukichochewa sana na mbunge wa Iringa, Peter Msigwa, ambaye ametuhumiwa kuendekeza zaidi maslahi yake ya kisiasa, badala ya maendeleo.
Kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo, miezi kadhaa iliyopita, madiwani kupitia kikao chao ambacho mbunge huyo ni mjumbe na alihudhuria, walikuwa wamekubaliana kuwa wamachinga hao watafutiwe sehemu nyingine kwa ajili ya kuendesha shughuli zao kila jumapili.
Chanzo cha kuhamishwa kwa wamachinga hao toka eneo la Mashine Tatu, kinaelezwa kuwa ni kutokana na ukweli eneo hilo lilikuwa linatakiwa kuachwa wazi kwa minajili ya kuwezesha ukarabati wa eneo hilo ambalo limekuwa korofi na hivyo kusababisha ucheleweshwaji wa ujenzi wa barabara ya Iringa Dodoma, mradi ambao umeshika kasi hivi sasa.
"Haya yalikuwa maamuzi ya Baraza la Madiwani, ambayo yaliwasilishwa kwa wamachinga hao na walikubali kuhamia eneo la Kitwilu, ambako walifanya biashara kwa majuma kadhaa, kabla ya kuanza kulalamikia ugumu wa biashara utokanao na kukosekana wateja na uduni wa miundombinu hasa ya kiafya" kimeeleza chanzo chetu kutoka eneo la tukio.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, baada ya hapo, wamachinga hao walikubaliwa kuhamishiwa sehemu ya Mlandege, ambayo iko kando kidogo ya mji. Huko walifanya biashara kwa muda na kukawa na ukimya hali ambayo iliashiria kuwa wameridhika na wangeendelea kufanya biashara zao huko.
Hata hivyo, katika hali ya kushangaza, inaelezwa kuwa katika moja ya mikutano yake, mbunge Msigwa, aliwaambia vijana hao kuwa warejee katika eneo la Mashine Tatu, kwakuwa yeye ni mbunge wao na kwamba halmashauri haikuwa na haki ya kuwafukuza mahali hapo.
"Hili ndilo linalolalamikiwa na wananchi na wanamtuhumu waziwazi mbunge kuwa amechangia sana machafuko ya leo. Yerye ni diwani kwa nafasi yake, anaingia vikao vya Baraza la Madiwani, anajua kile walichokuwa wameamua hapo awali, haieleweki imekuwaje tena akarejea na kuanza kuwatangazia wamachinga kurudi eneo ambalo awali walitakiwa kuondoka" amesema mwananchi mmoja aliyeongea na mwandishi wa habari hizi.
Kufuatia hatua hiyo, manispaa ililazimika kutoa tamko la kuwakataza wamachinga kurejea mahali hapo, hatua ambayo inaelezwa kuwa haikuweza pia kuafikiwa na mbunge, ambaye alirudia tena kuwataka wamachinga kurudi Mashine Tatu, kufanya biashara zao.
"Manispaa kwakuwa inajua kuwa ilishatoa tamko ambalo hata mbunge alihusika katika kuliandaa la kuwataka waondoke hapo, iliweka matangazo ya kuwakataza kufanya shughuli zao hapo, lakini pia kuweka ulinzi ili kudhihiti wale ambao wangekiuka agizo halali la kimamlaka, na walipokuja kufanya biashara leo, ndio ikawa kama hivi" ameeleza mwananchi mmoja toka eneo la tukio.
Mbunge amekamatwa?
Kwa mujibu wa taarifa ambazo zilikuwa bado hazijathibitishwa, mbunge Peter Msigwa, ambaye alikuwa akishiriki katika hafla ya kuchangia Harambee katika chuo kikuu cha Tumaini, alitembelea eneo la tukio hilo lakini ghafla akapotea tena kurejea Tumaini.
Hata hivyo, imeelezwa kuwa, mbunge huyo alikuwa amejisalimisha kwa Jeshi la Polisi baada ya kuambiwa kuwa anatafutwa kufuatia kuhusika kwake kuchochea vurugu hizo.
UPDATES ZITAKUWA ZIKIKUJIA
HAPA CHINI KUPITIA SANDUKU LA MAONI: Kama uko eneo la tukio, waweza pia
kututumia kile ulicho nacho kupitia info@jukwaahuru.com, WHATSAPP: +255
767 412176 au PIN: 290639AA
Picha zote hapo juu kwa hisani ya Blog ya The Choice.





























No comments:
Post a Comment