KAMPUNI
ya S. S. Bakhressa ilipoanzisha timu ya soka ya Azam FC, viongozi na mashabiki
wa klabu kongwe za Simba na Yanga walidhani ni nguvu ya soka.
S.
S. Bakhressa ikapiga hatua ya pili kwa kujenga uwanja wa kisasa, Chamazi,
Temeke, Dar es Salaam, ikiwa ni ishara ya dhamira ya kufanya mapinduzi ya soka
nchini.
Mbali
ya kujenga uwanja wa mazoezi (unatumika hata kwa mashindano) na uwanja mkubwa
wa kisasa ambao ujenzi wake ulizinduliwa na Rais Jakaya Kikwete hivi karibuni,
S.S. Bakhressa imeingia hatua nyingine kubwa kwa kuanzisha kituo cha
televisheni cha Azam TV.
Moja
ya malengo ya Azam TV inayojenga barabara ya Nyerere ni kutumia kiasi cha Sh.
1.5 bilioni kuonyesha moja kwa moja mechi za Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Ikiwa
itapata haki ya kuonyesha ‘live’ mashindano hayo, taarifa zinasema Azam TV
imejipanga kutoa Sh. 100 milioni kwa kila timu kati ya 14 zitakazoshiriki msimu
ujao wa ligi hiyo. Hii ni neema kubwa kwa klabu zote hasa changa.
Hii
ina maana sasa angalau kila timu, itaweza kujikimu kwa kiasi chake na kuweka
karibu uwiano sawa wa kuchuana na timu zenye uwezo mkubwa wa kifedha kama
Simba, Yanga na Azam FC iliyo chini ya kampuni ya S. S. Bakhressa.
Kwa
hiyo, timu zisizo na wadhamini mkubwa na ambazo ndiyo kwanza zimepanda daraja kama
Ashanti United ya Ilala, Mbeya City ya Mbeya na Rhino ya Tabora na hata
zilizopo kama Coastal Union zitanufaika kwa kiasi kikubwa na ujio wa udhamini
wa Azam TV.
Timu
zilizoshuka daraja za Toto African, African Lyon na Polisi Morogoro zitakuwa
zinasikitika neema kuja kwenye ligi wakati zimetupwa nje.
Msimu
uliopita tuliiona Toto ya Mwanza ikishiriki kwa tabu ligi hiyo huku wachezaji
wake wakilala katika basi wakati mwingine huku chakula pia kikiwa shida. Hali
hii inachangia kwa kiasi kikubwa timu hizi ambazo hazipo chini ya taasisi kubwa
kufanya vibaya hasa katika mechi zake za umbali mrefu na wakati mwingine hata
zile za katika kituo chake.
Kwa
vyovyote vile Azam TV inakuja kuleta ushindani mkubwa siyo katika udhamini tu,
bali hata urushaji wa vipindi vya michezo.
Lakini
Simba na Yanga zilizoanzishwa kabla ya uhuru ‘zinapanga’ hujuma. Simba wanadai kiasi
cha Sh. 100 milioni ni kidogo na hakilingani na hadhi yao na pia hawawezi
kulipwa sawa na timu nyingine za ligi hiyo.
Mwenyekiti
wa Simba, Ismail Rage amenukuliwa na gazeti moja la michezo akisema anakubaliana
na wazo la Azam TV, lakini kiasi hicho cha fedha ni kidogo kwao na hata siku
moja timu haziwezi kulipwa haki sawa ya matangazo huku akitolea mfano katika
Ligi Kuu ya England.
Kwa
upande wa Yanga, Ofisa Habari wake, Baraka Kizuguto amesema hawezi kuzungumzia
vitu vya tetesi kwani Azam TV hadi sasa hawajawapelekea taarifa rasmi kuhusu
lengo hilo la kuonyeshwa kwa mechi zao msimu ujao.
“Sipo
katika nafasi nzuri ya kuzungumzia jambo hilo, kwani hatujataarifiwa jambo
lolote juu ya mpango huo wa Azam TV, wakituletea maombi yao, sisi kama timu
tutakaa na kutoa uamuzi,” anasema Kizuguto.
Hii
ina maana kwamba, kama Simba na Yanga zitabaki na mawazo hayo, Azam TV inaweza
kukwamishwa katika mpango huu na kubaki na ule wa kuonyesha mechi za timu yao
tu, kwani lengo lao ni kutangaza biashara zao.
Utaratibu
ni kwamba muda ukifika, uongozi wa Azam TV utaomba kibali cha kudhamini Ligi
Kuu kutoka Kamati ya Ligi ambayo itapanga kiwango baada ya kuteta na klabu.
Vituo
vya TV vikionyesha ‘live’ mechi yoyote ya ligi hupaswa kulipa gharama kufidia
kiasi cha watu ambao hawataingia uwanjani na kutumia fursa hiyo kurusha
matangazo ya biashara. Azam TV haitazungumza na klabu binafsi.
Lakini
kwa desturi za Simba na Yanga, ambazo miaka nenda rudi ni kupanga mikakati ya
kuangushana, hata hili zinaweza kukwamisha. Kwa husuda zitaweka mgomo ili mpango
huu ufe ili zenyewe zibaki kutawala soka, timu ndogo zibaki zikinyanyasika kama
ilivyokuwa kwa Toto African iliyopigana hadi inashuka daraja.
Rai
yangu kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Kamati ya Ligi ni kwamba, Simba
na Yanga zisiachwe kuharibu mapinduzi ya soka yanayoletwa na Azam TV.
HABARI
HII IMETOLEWA KATIKA GAZETI LA MAWIO, IMEANDIKWA NA ELIUS KAMBILI


No comments:
Post a Comment