tuwasiliane

Saturday, May 4, 2013

AZAM KAZI NI KAZI LEO JIONI UGENINI





Baada ya kulazimishwa suluhu nyumbani mwezi uliopita, wawakilishi pekee wa Tanzania, Azam FC leo wataingia na kufanya mashambulizi kama nyuki wakati wanapowakabili FAR Rabat katika mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho CAF.
Sare yoyote ya mabao inatosha kwa Azam kufuzu kwa hatua nyingine ya mashindano hayo
“Tumekuja hapa Casablanca kumaliza kazi na vijana wangu wote wapo tayari kwa mchezo huu,” kocha wa Azam FC, Stewart Hall aliimbia MTNFootball.com.
“Soka siku hizi imebadilika sana, unaweza kushinda mechi sehemu yoyote iwe nyumbani au ugenini,” alisema Hall.
Alifafanua kuwa soka ya sasa hakuna kitu cha kujificha kwa sababu unachotakiwa kufanya ni kujiandaa kimbinu na kisaikolojia na ukiwa na bahati kidogo unaweza kushinda ugenini.
Azam iliyojihakikishia kucheza michuano hiyo mwakani ikiwa nafasi ya pili nyuma ya Yanga.
Leo itakuwa ikiwategemea washambuliaji wake mahiri Kipre Tchetche, John Bocco, Khamis Mcha na Mganda, Brian Umony ambao wamekuwa na rekodi nzuri ya kufunga kila mchezo katika hatua za awali.
Mshambuliaji Bocco ambaye katika mchezo wa kwanza alipoteza nafasi kadhaa za kufunga aliimbia MTNFootball.com kuwa lengo lake ni kufunga bao katika mchezo huo.
“Tumekuja kucheza kama timu na lengo letu ni moja tu kushinda,” alisema Bocco.
Naye Umony aliyeukosa mchezo wa kwanza kutokana na kuwa majeruhi, alisema wamedhamiria kufuzu kwa hatua ya tatu.
“Hatujawadharau Wamorocco, lakini tumejiwekea malengo ya kuona tunawatupa nje ya mashindano,” alisema Umony.
Hata hivyo, wenyeji wakiwa na nyota wao Moammed Al Bakar hawatakuwa tayari kuona wakifungashwa virago mbele ya mashabiki wao.
Azam FC ilichapa Barrack YC ya Liberia kwa jumla ya mabao 2-1 katika raundi ya pili baada ya kuisambaratisha timu ya Al-Nasir ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 8-1.

No comments:

Post a Comment