SHIRIKISHO
la Soka Tanzania (TFF) limemtaka mshambuliaji Nsa Job Mahenya wa
Coastal Union kuwasilisha maelezo yake juu ya madai kuwa alipewa rushwa
ya sh. milioni mbili ili asiifunge moja ya timu vigogo vya soka nchini.
Ofisa
Habari wa TFF, Boniface Wambura Mgoyo amesema leo kwamba, Job
alikaririwa Aprili 3 mwaka huu na kituo cha redio cha Clouds FM katika
kipindi cha Amplifier kuwa alipewa kiasi hicho cha fedha na kiongozi wa
timu husika ili asiifunge katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom, lakini
alipokea fedha hizo na kuifunga timu hiyo.
Wambura amesema lakini Nsa alilalamika baadaye kiongozi huyo alikuwa akimtaka arejeshe fedha hizo.
Amesema
pia TFF imekiandikia kituo hicho cha redio kutaka nakala ya kipindi
hicho ili pamoja na maelezo ya mshambuliaji huyo vipelekwe katika Kamati
ya Nidhamu kwa ajili ya hatua za kinidhamu.
“TFF
itachukua hatua kali dhidi ya Job iwapo hatawasilisha maelezo yake
kuhusiana na suala hilo, na imetaka wadau kutoa ushirikiano ili iweze
kupambana kikamilifu na vitendo vya rushwa kwenye mpira wa
miguu,”amesema.
TFF inaonekana kuanza kuvalia njuga madai kuhusu rushwa katika soka ya Tanzania, baada ya kufumbia macho kwa muda mrefu.
Kipa
Shaaban Kado wa Coastal, wakati akiwa Mtibwa Sugar aliwahi kudai
kupelekewa fedha na mshambuliaji wa zamani wa Simba SC, Ulimboka
Mwakingwe, aliyetumwa na kiongozi wa Wekundu hao wa Msimbazi, ili aachie
mabao katika mechi baina ya timu hiyo.
Hata hivyo, pamoja na suala hilo kufikishwa kwenye vyombo vya sheria hakuna hatua zaidi zilizowahi kuchukuliwa.
Wachezaji
wanne wa Azam FC, kipa Deo Munishi ‘Dida’ na mabeki Erasto Nyoni,
Aggrey Morris na Said Mourad wa Azam FC, kwa sasa wamesimamishwa na
klabu yao, kwa tuhuma za kuihujumu timu hiyo dhidi ya Simba katika
mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ikafungwa 3-1.
Lakini suala la wanne hawa kwa sasa lipo kwenye meza ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
No comments:
Post a Comment