KOCHA wa Simba, Mfaransa Patrick Liewig ameweka wazi kuwa atawapa kipaumbele chipukizi katika mechi zake nane zilizobaki za Ligi Kuu Bara kwa kuwa wazoefu hawako fiti kama anavyotaka.
Liewig alisisitiza kuwa anawarudisha wachezaji wazoefu wote kwenye mazoezi ya gym ambayo atakuwa akiwafanyisha mara mbili kwa wiki.
Baadhi ya wachezaji wazoefu wanaocheza kwenye kikosi cha Simba ni Amri Kiemba, Mrisho Ngassa, Mwinyi Kazimoto, Ramadhani Chombo 'Redondo', Juma Kaseja, Mudde Mussa na Haruna Moshi 'Boban'.
Mbali na hivyo kocha huyo amewataka wadau wa Simba kusahau yaliyopita na kuelekeza nguvu zao katika mechi za Ligi Kuu Bara zijazo ili wapate nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa.
Simba ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 31 sawa na Mtibwa na Coastal Union, Yanga ndiyo vinara wana pointi 42.
Liewig alisema: "Kutokana na wachezaji wazoefu kutokuwa fiti, nitatoa nafasi kwa chipukizi kwa ajili ya maendeleo ya timu kwa sasa na baadaye, nimewajumuisha vijana saba ambao nitakuwa nao," alisema.
Vijana hao ni Miraji Madenge, Ramadhani Singano na Rashid Ismail (winga na washambuliaji), Said Ndemka (kiungo) Emily Mgeta, Miraji Adam na Hassan Isihaka (mabeki).
Mbali na hao Simba ina chipukizi wengine ambao ni Harun Chanongo (winga), Abdalah Seseme (kiungo), Hassan Khatib (beki) na Abou Hashim (kipa).
Kuhusu mechi ya Coastal Union kesho Jumapili, Liewig alisema itakuwa vizuri: "Tuna wakati mgumu kutokana na nafasi tuliyopo kwa sasa lakini pia tuna mechi ngumu kama ya Yanga na Azam ambayo tunatakiwa kushinda, tunaomba mashabiki watuunge mkono timu ipate nguvu, wasikate tamaa,"alisema.
No comments:
Post a Comment