MAKAMU
Mwenyekiti wa Simba SC, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ inadaiwa amemuandikia
barua pepe, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Alhaj Ismail Aden Rage kumtaarifu
kujiuzulu wadhifa huo.
Habari
ambazo CHANZO CHETU Kimezipata jioni hii zimedai kuwa, Kaburu
amemuandikia barua pepe Rage, ambaye kwa sasa yupo India kwa matibabu ya
mgongo kumjulisha uamuzi wake huo.
Juhudi za kumpata Kaburu mwenyewe kuzungumzia habari hizo, hazikufanikiwa kutokana na simu zake zote kutopatikana.
Kaburu
anakuwa kiongozi wa pili wa Kamati ya Utendaji ya Simba kujiuzulu leo,
baada ya awali mchana, Zacharia Hans Poppe aliyekuwa Mjumbe kujiuzulu
pia.
Hans
Poppe, aliyekuwa pia Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, alisema kwamba
ameamua kujiuzulu nyadhifa zote hizo kwa sababu kuna mgawanyiko ndani ya
uongozi unaokwamisha maendeleo.
Akizungumza
na CHANZO CHETU ofisini kwake jioni ya leo Mbezi Beach, Dar es Salaam,
Hans Poppe alisema kwamba kwa kuona hawapati mafanikio wanayoyatarajia,
ameamua kung’atuka kuwapisha wengine.
“Kwa
muda wa takriban miaka mitatu sasa nimekuwa nikishikilia nyadhifa ndani
ya Simba. Nimejitahidi kutekeleza majukumu yangu kadiri ya uwezo wangu,
lakini naona hatupati mafanikio tunayoyatarajia, ”alisema.
“Ni
wazi kuwa kwenye uongozi tumekuwa hatufanyi kazi kwa umoja na
mgawanyiko huu unatukwaza na hatuwezi kupata maendeleo,”alisema Hans
Poppe.
“Baada
ya kutafakari, nimeona ni bora nijiuzulu nyadhifa hizo kupisha wengine
ambao wanaweza wakawa na mawazo mapya ya kuendeleza klabu, nami
nitabakia kuwa mwanachama mwaminifu daima,”alisema Hans Poppe.
Poppe
amewasilisha barua ya kujiuzulu Simba SC leo na wazi kujiuzulu kwa
Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) ni pigo kwa
klabu hiyo, kwani alikuwa akiisaidia mno kwa hali na mali.
Aidha,
kujiuzulu kwa Hans Poppe wazi kutachochea zaidi mgogoro ndani ya klabu
hiyo na kuongeza shinikizo la viongozi wa klabu hiyo kujiuzulu pia.
Simba
SC kwa sasa haifanyi vizuri katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na
tayari imekwishatolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kufungwa
jumla ya mabao 5-0 na Recreativo de Libolo ya Angola katika raundi ya
kwanza tu.
Ubingwa
wa Ligi Kuu ni kama umekwishaota mbawa, kwani hadi sasa Wekundu hao wa
Msimbazi wanashika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 31, sawa na Coastal
Union ya Tanga na Mtibwa Sugar ya Morogoro, nyuma ya Azam FC yenye
pointi 36 na Yanga inayoongoza kwa pointi zake 42, zote za Dar es
Salaam.
No comments:
Post a Comment