tuwasiliane

Monday, March 11, 2013

ICC yatupilia mbali kesi dhidi ya Muthaura

Mahakama ya kimataifa ya ICC inatupilia mbali kesi ya uhalifu dhidi ya binadamu iliyokuwa inamkabili aliyekuwa mkuu wa utumishi wa umma nchini Kenya Francis Muthaura.
Hii ni baada ya shahidi mkuu katika kesi hiyo kusema alitoa ushahidi wa uongo.
Muthaura alihusishwa na ghasia za baada ya uchaguzi Kenya mwaka 2007 kwa kuwa mmoja wa wale waliopanga na kufadhili mashambulizi ya uklipza kisasi dhidi ya jamii moja.
Kiongozi wa mashtaka, Fatou Bensouda alisema anafutilia mbali mashtaka yote dhidi ya Francis Muthaura ambaye anatuhumiwa kwa uhalifu ikiwemo mauaji na ubakaji baada ya kutokea dosari katika ushahidi.
Wakati huohuo mawakili wa rais mteule wa Kenya Uhuru Kenyatta nao wanatarajia baadaye leo kuwashawishi majaji katika mahakama hiyo kudurusu ushahidi ambao viongozi wa mashtaka walitoa dhidi ya Kenyatta kwa tuhuma kuwa alihusika na ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007
Mawakili wa Kenyatta wanatarajiwa kutoa hoja yao siku mbili baada ya Kenyatta kushinda uchaguzi wa urais , wa kwanza kufanyika tangu ghasia za baada ya mwaka 2007.
Mawakili wanasema majaji wanapaswa kudurusu kesi hiyo hasa baada ya shahidi mmoja kutoa ushahidi wa uongo na hivyo kuhujumu kesi dhidi ya Uhuru na mshukiwa mwingine Francis Muthaura.
Kenyatta alishinda uchaguzi wa wiki jana licha ya kesi anayokabiliwa nayo katika mahakama ya ICC kwa kosa la uhalifu dhidi ya binadamu, ikiwemo mauaji, ubakaji na kuwalazimisha watu kuhama makwao.
Viongozi wa mashtaka wanamtaja kama mmoja wa wahusika katika ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007.
Kenyatta, ambaye ni mwanawe rais mwanzilishi wa Kenya, Jomo Kenyatta ni mmoja wa watu matajiri wakubwa zaidi barani Afrika na anasisitiza kuwa hana hatia.
Kesi dhidi ya Kenyatta itaanza mwezi Julai

source. bbc

No comments:

Post a Comment