Siku moja baada ya kuiongoza timu ya
Taifa ya Tanzania kuitandika Morocco 3-1 na kujiweka kwenye nafasi nzuri
kwenye michuano ya kugombania nafasi ya kushiriki michuano ya kombe la
dunia 2014. Leo serikali kupitia naibu waziri wa michezo na habari
Mh.Amos Makalla imesema itaendelea kumlipa mshahara kocha wa timu ya
taifa Kim Poulsen.
Kim Poulsen ambaye alichukua nafasi ya
Jan Poulsen mwaka jana kuiongoza timu ya soka ya wakubwa ya Tanzania,
amekuwa na rekodi nzuri katika kuiongoza timu ya taifa kwenye kipindi
kifupi alichokaa huku timu ikionyesha mwelekeo mzuri kwa kufanya vizuri
kwenye michuano mbalimbali inayoshiriki.
Akizungumza na mtandao huu asubuhi ya
leo Mh.Amos Makalla alisema: "Naipongeza sana Taifa Stars kwa ushindi
walioupata, nawapongeza wachezaji kwa kujituma muda wote hakika
wameijengea heshima Tanzania nawataka waongeze bidii wasibweteke!
Nampongeza kocha mkuu na benchi la ufundi kwa muda mdogo ameijenga timu
vizuri na amewaelewa wachezaji vizuri. Nawashukuru watanzania kwa
kujitokeza kwa wingi na kuishangilia timu yao muda wote, aidha serikali
inakusudia kuunda kamati ya kusaidia Taifa Stars ili kuongeza nguvu
haraka iwezekanavyo ili kuiwezesha kufanya vema katika mechi zilizobaki!
Pamoja na kamati serikali itaendelea kulipa mishahara wa kocha wa timu
ya taifa." - alimaliza Makalla

No comments:
Post a Comment