tuwasiliane

Saturday, February 2, 2013

BIN KLEB AZUNGUMZIA TUHUMA ZA WACHEZAJI YANGA KUPIGANA MISUMALI

Bin Kleb kulia akizungumza na Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub 'Cannavaro'

MWENYEKITI wa Kamati ya Mashindano ya klabu ya Yanga SC, Abdallah Ahmad Bin Kleb amesema kwamba hakuna suala la ushirikina ndani ya klabu yao, bali kuna watu ambao ni wapinzani wao wanapandikiza chuki kwa wachezaji wao, ili kuvuruga umoja na amani iliyopo ndani ya kikosi chao kwa sasa.
 
Akizungumza na CHANZO CHETU jana, Bin Kleb alisema kwamba amesikia wapo wachezaji walitaka kushikana mashati mazoezini wakituhumiana kulogana, lakini baada ya uongozi kulifanyia kazi suala hilo, umegundua kuna watu wanapandikiza chuki baina ya wachezaji wao hao.
 
Mshambuliaji Mrundi, Didier Kavumbangu anadaiwa kumvaa Jerry Tegete na kumtuhumu kwamba anamloga kumpunguza kasi uwanjani, ili ang’are yeye.
“Hakuna kitu kama hicho, kuna watu wanawachonganisha hawa wachezaji, wewe fikiria sasa wao ndio wanacheza kama washambuliaji pacha na wanaelewana sana, hakuna anayekaa benchi kati yao, sasa hilo suala la kulogana linatoka wapi?”alihoji Bin Kleb.
 
Kiongozi huyo alisema jambo ambalo anaweza kukiri ndani ya Yanga hivi sasa ni  ushindani mkubwa wa namba ndani ya kikosi kizima na ili mchezaji apate nafasi kwenye kikosi cha kwanza, lazima afanye kazi haswa.
 
“Tumezungumza nao wachezaji na tutaendelea kuzungumza nao, wanapaswa kuwa makini, mtu kama hafanyi vizuri atafute sababu za msingi za kitaalamu na si kutuletea mambo ya Kiswahili kwenye timu.
 
Leo ukipandikiza chuki eti Tegete anamloga Kavumbangu, kwa sababu Tegete anafunga na Kavumbangu hafungi, je wakati wa mzunguko wa kwanza Kavumbangu alipokuwa anafunga Tegete hafungi, nani alikuwa anamloga mwenzake?”alihoji Bin Kleb.
 
Kiongozi huyo amesema kwamba wanapocheza washambuliaji wawili kama pacha lazima mmoja ndiye awe anafunga sana na wengine watafunga zikitokea nafasi. “Angalia hata Manchester United, Wayne Rooney ndiye alikuwa mfungaji wa timu, lakini kasajiliwa Van Persie mambo yamebadilika. Van Persie ndiye anafunga sana sasa hivi, ikitokea Rooney akapata nafasi naye anafunga. Huwezi kusikia mtu Analia kalogwa,”alisema Bin Kleb.
 
Kleb amewaasa wachezaji wa Yanga kuwa makini na watu wenye lengo la kuwachonganisha kuvuruga amani iliyopo ndani ya kikosi chao kwa sasa ambayo ndiyo siri ya mafanikio yao, ikiwemo kutwaa Kombe la Kagame, kuongoza Ligi na kwa ujumla kufanya vizuri.
 
“Tunaelekea kuzuri, sasa vema wachezaji wetu wakatuliza sana akili zao na kuwa makini na adui zetu, wanaotaka kuwavuruga ili timu ishuke kiwango,”alisema.
Yanga inatarajiwa kushuka dimbani tena leo kucheza mechi ya pili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro, mchezo ambao utafanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mchezo wake wa kwanza, Yanga ilishinda 3-1 dhidi ya Prisons ya Mbeya na kuzidi kujichimbia kileleni mwa ligi hiyo, baada ya kufikisha pointi 32, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 30 na Simba pointi 26. Ikumbukwe, katika mechi yha mzunguko wa kwanza, Yanga ilifungwa 3-0 na Mtibwa mjini Morogoro.    

No comments:

Post a Comment