BIASHARA
imeisha. Azam FC imemuuza Mrisho Khalfan Ngassa kwa dola za Kimarekani 75,000
kwenda El Merreikh ya Sudan ambako amesaini mkataba wa miaka miwili,
utakaomuwezesha kulipwa mshahara wa dola za Kimarekani 4,000 kwa mwezi huku naye
akilipwa dola 50,000 za kusaini.
Awali,
Merreikh walitaka kumpa mkataba wa miaka mitatu Ngassa wenye thamani ya dola
100,000, lakini wakala wake Alhaj Yussuf Said Bakhresa akakataa akisema
utambana mchezaji wake aking’ara na kutakiwa na klabu nyingine.
Sasa Ngassa
baada ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge mwishoni
mwa wiki hii, atakwenda Sudan kufanyiwa vipimo tayari kujiunga na klabu hiyo, ambayo
ni jambo la kawaida kucheza hatua ya makundi ya michuano ya klabu Afrika.
Azam FC
imesema imeweka mbele maslahi ya mchezaji na taifa kwa ujumla katika maamuzi ya
kumuuza Sudan, kutoka Simba alikokuwa akicheza kwa mkopo. “Hii timu (Merreikh)
kila mwaka inacheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, maana yake
huyu mchezaji atakwenda kupata maendeleo na kuja kuisaidia zaidi Tanzania
katika mashindano ya kimataifa,”alisema kiongozi mmoja wa Azam.
Alipoulizwa kuhusu
Simba SC aliyokuwa anaichezea klabu hiyo, kiongozi huyo alisema wao walimtoa
kwa mkopo Ngassa kwenda kwa Wekundu wa Msimbazi hadi Mei 31, mwakani na mkataba
wao ndio unasema hivyo.
“Sisi
tuliwapa Simba huyu mchezaji kwa mkopo hadi Mei 31 na wakatupa Sh. Milioni 25,
ila tuko tayari kuwarudishia fedha zao walizota, lakini huyu mchezaji ni mali
yetu na hata TFF wanatambua hilo, na
tumekwishamuuza Merreikh,”alisema.
Alipoulizwa kuhusu
Simba kusaini mkataba mpya na Ngassa, alisema; “We uliona wapi dunia nzima timu
inapewa mchezaji kwa mkopo halafu inamsainisha mkataba? Simba lazima ifike
wakati waache kurudia makosa, haya ndio mambo ya Mbuyu Twite sasa,”alisema
kiongozi huyo wa Azam.
Katika kukamilisha
mauzo ya mchezaji huyo, kiongozi wa Marreikh akiwa Dar es Salaam mbele ya
viongozi wa TFF na Azam, alipigiwa simu Ngassa aliye hapa Kampala, Uganda na
kuhusishwa katika dili hilo, naye akakubali ndipo mambo yakamalizwa.
Aidha, Azam wameomba
TFF ihakikishe kunakuwa na ulinzi katika kambi ya timu ya taifa mjini hapa, ili
Simba wasimfanyie vurugu Ngassa na kumvuruga kisaIkolojia, wakati ndiyE tegemeo
la timu katika kampeni ya kutwaa Kombe la Challenge mwaka huu mjiini hapa.
Kwa upande
wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe
akizungumza kutoka Dar es Salaam, alisema kwamba watawapeleka mahakamani Azam kwa
kitendo cha kumuuza mchezaji wao kinyume cha sheria.
“Haiwezekani
wamuuze wao, wakati wao walituuzia huyu mchezaji na sisi tuna mkataba ambao
tulisaini nao, hii ni kinyume cha sheria na sisi tutawapeleka mahakamani,”alisema
Hans Poppe ambaye anatua kesho mjini hapa.
Azam
walimtoa kwa mkopo Ngassa mwanzoni mwa Agosti, mwaka huu baada ya kukerwa na
kitendo cha mchezaji huyo kubusu jezi ya timu yake ya zamani, Yanga, katika
Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, dhidi
ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Alifanya
hivyo, baada ya kufunga bao la ushindi akitokea benchi na kuiwezesha Azam
kutinga fainali ya michuano hiyo, ambako walifungwa na Yanga 2-0, naye kwa mara
nyingine akitokea benchi na kushindwa kufunga, hivyo kutuhumiwa kucheza kinazi.
Ilielezwa
kwamba Simba walitoa Sh. Milioni 25 kumnunua kwa mkopo mchezaji huyo, ingawa
baadaye Simba wakasema waliununua mkataba wa mwaka mmoja aliobakiza mchezaji
huyo Azam FC, nao wakamuongezea wa mwaka mmoja kwa kumsainisha kwa Sh. Milioni
30, kati ya hizo Milioni 12 akipewa taslimu na 18 akipewa gari.
No comments:
Post a Comment