SIKU moja baada ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete kutangaza safu
mpya ya wajumbe wa Sekretarieti ya chama hicho, wasomi, wanasiasa na
viongozi wa dini wameponda uteuzi huo wakisema chama hicho tawala,
kisitarajie jipya kutoka katika safu hiyo.
Wakizungumza kwa
nyakati tofauti na CHANZO CHETU, wadau hao walisema viongozi
walioteuliwa wana upungufu, hivyo hawawezi kuwajibishana kwa kuwa
wanaogopa kuumbuana.
Katika uteuzi huo Kikwete aliwateua,
Abdulrahaman Kinana kuwa Katibu Mkuu wa CCM, akisaidiwa na Mbunge wa
Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba upande wa Bara na Vuai Ali Vuai upande
wa Zanzibar.
Wengine ni Zakhia Meghji aliyeteuliwa kuwa Katibu
wa Uchumi na Fedha, Mohamed Seif Khatib (Oganaizesheni), Dk Rose Migiro
(Kimataifa) na Nape Nnauye (Uenezi).
Uteuzi huo ulitanguliwa na
uchaguzi ambao ulimrejesha Kikwete kuwa Mwenyekiti wa chama wa Taifa
akisaidiwa na Philip Mangula (Tanzania Bara) na Dk Ali Mohamed Shein
(Zanzibar).
Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa
wanawatizama Mangula na Kinana kama viongozi makini, lakini wasioweza
kumudu kasi ya siasa za sasa ambazo zimebadilika kulingana na wakati na
aina ya ushindani kutoka upinzani.
Kadhalika wanakiona kikosi
hicho kuwa hakiwezi kuisaidia CCM kupambana na rushwa, ambayo inaonekana
kuota mizizi kiasi cha kuonekana kama sehemu ya utamaduni wa chama
hicho.
Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Bukoba,
Methodius Kilaini alisema safu hiyo ya uongozi haina jipya akifafanua
kuwa, tatizo kubwa la chama hicho ni mfumo wake wa utendaji kazi.
“Ni mfumo ambao wamejiwekea wa kulindana, hivyo uongozi huu hautaleta mabadiliko yoyote CCM,” alisema Kilaini.
Alisema
viongozi waliochaguliwa hawatakuwa na sauti kwa kuwa nao wana udhaifu
wao hivyo hawawezi kuwachukulia hatua wenzao kwa kuwa nao wataumbuliwa.
Askofu Kilaini alisema viongozi hao wataendeleza mfumo walioukuta na hakuna atakayeweza kumkosoa mwenzake aliyefanya makosa.
“Kati
ya viongozi wa CCM waliochaguliwa hakuna atakayemnyooshea mwenzake
kidole kwamba amefanya kosa fulani, ni vigumu mno kumwadhibu mwenzake
kwa kuhofia kuwa, kwa vile yeye pia ni dhaifu akimwadhibu huyo matendo
yake yatagundulika,” alisema.
Alisema licha ya Rais Kikwete
kukemea rushwa kwa viongozi wote waliochaguliwa, lakini hakuna hatua
yeyote aliyochukuwa kwa wale waliotuhumiwa kujihusisha na vitendo hivyo
wakati wa chaguzi za ndani ya CCM.
“Rais wetu anazungumzia
rushwa na kukemea lakini hakuna aliyemchukulia hatua yoyote kwa wale
waliokutwa wakitoa rushwa katika uchaguzi wa Umoja wa Vijana (UVCCM),
Jumuiya ya Wazazi na Ujumbe wa Halmashauri Kuu (Nec),” alisema Kilaini.
Kauli za wasomi
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Kitila Mkumbo alisema
Watanzania wasitegemee mabadiliko katika safu mpya ya uongozi ya CCM kwa
kuwa walioteuliwa hawana jipya.
“Mangula ni kiongozi mwenye sifa
nzuri kutokana na kusimamia misingi ya TANU ndani ya CCM, ila msimamo
wake hauwezi kufanikiwa katika kipindi hiki kwa sababu sura ya chama ni
tofauti na mtizamo alionao,” alisema Dk Mkumbo.
Alisema Kinana
licha ya kushika nafasi mbalimbali ndani ya CCM tangu utawala wa
Serikali ya awamu ya tatu, lakini hakuweza kuleta mabadiliko yoyote
ndani ya chama hicho.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma
(UDOM), Profesa Idris Kikula alisema utendaji kazi wa viongozi hao wapya
hauwezi kutabiriwa kwa sasa, kwani ni mapema mno.
Alisema kuwa,
viongozi hao wanatakiwa kupewa muda wa kufanya kazi zao na kwamba
kuwasema kwa sasa ni sawa na kuwahukumu bila kosa lao.
Profesa
Kikula alisema kuwa, aliufuatilia kwa makini uchaguzi huo na kubaini
kuwa jambo lililotakiwa kufanyiwa kazi zaidi ni tuhuma za rushwa
zinazowakabili baadhi ya makada wa chama hicho.
Mhadhiri wa Chuo
Kikuu cha Mzumbe, Dk George Shumbusho alisema licha ya baadhi ya
viongozi hao kuwa na sifa nzuri, changamoto inayowakabili ni kutokomeza
rushwa ndani ya chama hicho tawala.
“Mangula na Kinana ni
viongozi wazuri, ila hawawezi kuleta mabadiliko bila ya kupata
ushirikiano kutoka kwa wanachama wengine, mzigo mkubwa walionao ni
kuhakikisha kwamba wanaondoa tatizo la rushwa,” alisema Shumbuso.
Shumbusho
alisema kuwa kama CCM haitachukua uamuzi mgumu kwa wanachama wake bila
kujali urafiki, haitaweza kumaliza tatizo la rushwa na itaendelea
kupigiwa kelele na wapinzani na wananchi.
Ofisa Elimu Mwandamizi
wa chuo kikuu Kishiriki cha Elimu cha Dar es Salaam (Duce), Simon Shayo
yeye alisema: “Sidhani kama kuna mabadiliko yatakayojitokeza ndani ya
CCM kwa sababu viongozi ni walewale, changamoto ndani ya chama hiki
haziwezi kuondolewa na wazee hata kama baadhi yao wanaonekana kuwa na
sifa.”
Shayo alisema kipindi hiki kilikuwa ni nafasi ya vijana
kupewa nafasi ya kuleta mabadiliko ndani ya chama hicho kwa sababu ndiyo
wenye nia ya dhati ya kukiletea mabadiliko.
Wanasiasa
Katibu
Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema kuwa safu hiyo mpya haiwezi
kupambana na ufisadi na kutekeleza dhana ya kujivua gamba kwani wengi ni
watuhumiwa wa ufisadi.
Alitoa mfano wa kashfa ya wizi wa
mabilioni ya Fedha za Akaunti ya Nje (EPA) kutoka Benki Kuu (BoT) na
utoroshaji wa nyara na fedha za umma nje ya nchi, alisema uteuzi huo
umelenga kufukia madhambi ya ufisadi unaowakabili viongozi wengi kwenye
chama hicho na serikalini.
Katika maelezo yake Dk Slaa
ukiwachunguza viongozi hao mmojammoja utabaini kwamba kila mmoja ana
matatizo yake ya kutuhumiwa katika jambo moja au jingine na kwamba
katika mazingira ya aina hiyo, hakuna matumaini ya kuwapo kwa
mabadiliko.
“Ni kwa sababu tu watu wanasahau, naona watu wanasema
hiyo ni safu mpya, wengine wanasema safu ya ushindi, mimi nasema hakuna
upya wowote hapo, wala hakuna safu ya ushindi,” alisema Dk Slaa na
kuongeza;
“Safu hiyo imeundwa ili kuendelea kulinda ufisadi ambao
umeendelea kukididimiza chama hicho na Serikali yake, lengo ni kufukia
na kupanga mikakati ya kufanikisha ufisadi mwingine kwa ajili ya
kuendelea kuwa madarakani kwa CCM.”
Alisema kuwa ili Watanzania waweze kupiga hatua, taifa linatakiwa kuwa na viongozi ambao hawahusishwi na kashfa za ufisadi.
Kwa
upande wake, Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Samwel Ruhuza alisema hakuna
jipya katika sekretarieti hiyo mpya licha ya kuwarudisha wakongwe.
“Nilitegemea
vijana wangepewa nafasi kubwa katika uteuzi huo kwa kuwa hivi sasa
vijana ndiyo chachu ya ushindi katika kila chama, halafu wakongwe
wakabaki washauri, lakini imekuwa sivyo,” alisema Ruhuza.
Naye
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Julias Mtatiro alisema
kuwa, watu ni walewale walioteuliwa kushika nafasi hizo hivyo hakuna
mabadiliko yoyote yatakayokea.
“Sidhani kama uteuzi huo utasaidia
kuleta maendeleo katika chama chao na hata katika taifa kwa sababu
ndicho chama tawala,” alisema Mtatiro na kuongeza;
“Wote walioteuliwa walishawahi kushika nafasi za juu katika Serikali kupitia chama hicho, hivyo hakuna jipya walilofanya”.
Imeandaliwa na Bakari Kiango, Fidelis Butahe, Kelvin Matandiko, Peter Elias, Magreth Munisi na Pamela Chilongola.
SOURCE; GAZETI LA MWANANCHI
No comments:
Post a Comment