MICHUANO ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati,
CECAFA Tusker Challenge 2012 inatarajiwa kuendelea leo kwenye Uwanja wa
Mandela, Namboole wakati timu ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars itakapojitupa
dimbani kumenyana na Burundi, Int’hamba Murugamba.
Stars, inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, inahitaji
ushindi katika mchezo wa leo utakaoanza saa 12:00 jioni, ili kujihakikishia
kutinga Robo Fainali, baada ya awali kushinda mabao 2-0 dhidi ya Sudan.
Stars itamenyana na Burundi, ambayo inaongoza Kundi B kwa
wastani wa mabao, japokuwa inalingana kwa pointi na Bara. Kabla ya mechi hiyo,
Somalia wanaoshika mkia katika kundi hilo, watamenyana na Sudan kuanzia saa
10:00 jioni.
Kocha
wa Kilimanjaro Stars, Mdenmark Kim Poulsen amesema kwamba uwezo wa timu yake
unazidi kukua siku hadi siku na sasa ana matumaini ya kufanya vizuri zaidi
katika michuano hii.
“Tuliwafunga
Kenya (mchezo wa kirafiki Mwanza), tumewafunga Sudan, timu zote nzuri, Sudan
wapo juu yetu kiuwezo katika viwango vya FIFA. Kwangu siangalii sana viwango
vya FIFA, mpira ni pale unapokuwa uwanjani,”alisema Poulsen.
Akilizungumzia
kundi lake, B lenye timu za Sudan, Somalia na Burundi, alisema ni gumu na
wanatakiwa kupambana ili kufika mbali.
Lakini
Poulsen amesema bado anawahitaji mno washambuliaji Mbwana Ally Samatta na
Thomas Emanuel Ulimwengu wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
(DRC) , ambao wamezuiwa na klabu yao.
Kim alisema
jitihada za kuwaomba Mazembe wawaruhusu wachezaji hao zinaendelea.
“Sijui
itakuwaje wasipokuja, itanibidi tu niwatumie wachezaji hawa hawa waliopo, najua
nina mshambuliaji mmoja, lakini nitawatumia hawa hawa waliopo, Simon Msuva
anaweza akawa mshambuliaji, nitafanyeje,”.
“Siwezi
kuita mchezaji mwingine kutoka nyumbani kwa sasa, kwa sababu mtu lazima umuone
uwezo wake, huwezi kumuita tu, kwa hivyo naomba Mungu tu Samatta na Ulimwengu
waje,”alisema Kim.
Katika
mchezo wa leo, Kim ambaye amekuwa akifuatilia kwa makini mashindano haya ili
kujua uwezo wa timu zote, hatarajiwi kuwa na mabadiliko kwenye kikosi chake
kutoka kile kilichoifunga Sudan 2-0.
Kama
kawaida, Nahodha Juma Kaseja anatarajiwa kuanza, kulia akicheza Erasto Nyoni,
kushoto Amir Maftah na mabeki wa kati, Kevin Yondan na Shomary Kapombe. Kiungo
mkabaji Frank Domayo, wingi ya kulia Simon Msuva, kushoto Mrisho Ngassa kiungo
mchezeshaji Salum Abubakar na Mwinyi Kazimoto atacheza nyuma ya mshambuliaji
pekee, John Bocco ‘Adebayor’.
Mfumo wa
sasa Kim unaonekana kuwa na tija kwa Stars, kwani analundika viungo wengi, huku
akitumia mawinga ambao wanasababisha presha kubwa ya mashambulizi.
Leo kama
Bocco atakuwa makini anaweza kufunga zaidi ya mabao mawili aliyofunga kwenye
mchezo wa kwanza, kwani kama alivyosema timu inazidi kuimarika siku hadi siku.
No comments:
Post a Comment