tuwasiliane

Sunday, November 25, 2012

KILIMANJARO STARS KURUSHA KARATA YA KWANZA LEO

TIMU ya taifa ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars leo inatarajiwa kuanza kampeni zake za kuwania Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge leo itakapomenyana na Sudan kuanzia saa 12:00 jioni Uwanja wa Mandela, Namboole mjini hapa.
 
Mchezo huo, utatanguliwa na mchezo mwingine wa Kundi B kati ya Somalia na Burundi, kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja huo huo.
Kocha wa Kilimanjaro Stars, Mdenmark Kim Poulsen amesikitishwa na kutowasili kwa washambuliaji Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
 
“Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanaweza wasicheze katika mechi ya kwanza kwa sababu hawajafika, lakini mimi nikiwa kocha nimejiandaa vizuri na nina imani na wachezaji waliopo,” alisema.
 
“Nina imani TFF wanafuatilia suala hili na wachezaji hawa watajiunga na wenzao hivi karibuni lakini hii haituzuii kufanya vizuri kwani tumejiandaa vizuri,” alisema.
Alisema wachezaji wote wana hali nzuri na wana ari ya kushinda mechi yao ya kwanza dhidi ya Sudan ambazi zimo katika Kundi B pamoja na Burundi na Somalia ambazo zitacheza leo pia.
 
Hata hivyo, jana Kili Stars walilalamikia Uwanja mbovu wa Chuo Kikuu cha Kampala Kampasi ya Biashara, waliopelekwa kufanya mazoezi kujiandaa na mechi ya leo.
 
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniphace Wambura aliwasilisha malalamiko hayo kwa Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Uganda (FUFA), Rodgers Mulindwa ambaye ameahidi kuyafanyia kazi.
“Tutalifanyia kazi suala hilo, tutakuwa na kikao kesho (leo) litawasilishwa na litapatiwa usumbufu, mwanzo huwa na matatizo, lakini mambo yatakuwa mazuri,”alisema Mulindwa.
 
Hata hivyo, inashangaza Stars kupelekwa katika Uwanja wa Chuo Kikuu cha Kampala Kampasi ya Biashara, wakati kwenye mpango wa awali kabisa wa FUFA ilitakiwa kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Nakawa.   

No comments:

Post a Comment