tuwasiliane

Sunday, October 14, 2012

Pesa za Twite bado moto

HUKU Klabu ya Simba ikiendelea kuishinikiza Yanga kuwalipa pesa za usajili wa mchezaji Mbuyu Twite, Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), inajiandaa 'kuihukumu' klabu hiyo ya Jangwani kwa kushindwa kutekeleza agizo walilowapa.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Alex Mgongolwa amesema wanatarajia kukutana wakati wowote kuanzia sasa kujadili hatua za kuchukuliwa dhidi ya Yanga.

Septemba 10 mwaka huu, kamati hiyo ilimuidhinisha Twite kuichezea Yanga, lakini ikiitaka klabu hiyo ya Jangwani kurejesha Simba pesa kiasi cha dola 32,000 alizochukua mchezaji huyo alipoingia mkataba na Simba.

Kamati hiyo pia iliitaka Yanga kumaliza pesa za usajili wa mchezaji David Luhende kutoka Kagera Sugar ndani ya siku hizo 21, lakini mpaka sasa hawajafanya hivyo.

Mgongolwa alisema kamati yake imemwandikia barua Katibu wa TFF, Angetile Osiah kumtaka aitishe kikao ili kujadili suala hilo.

Afisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema wameshangazwa hatua ya Yanga kukaidi kulipa pesa hizo kama walivyoelekezwa na kamati.

"Tuliiandikia barua TFF Septemba 29 mwaka huu kuwaomba waikate Yanga fedha kwenye mechi yetu na wao ili kufidia deni hilo, lakini TFF hawakufanya hivyo," alisema Kamwaga.

Kaimu Katibu wa Yanga, Lawrance Mwalusako alikerwa na swali aliloulizwa kuhusu lini klabu hiyo itakuwa tayari kulipa madeni fedha hizo.

"Hili ni suala la kiungozi zaidi, siyo jukumu lenu kufahamu, nachofahamu watakamalizana wenyewe," alisema Mwalusako.

Wakati huohuo, wadhamini wa Ligi Kuu Bara, Kampuni ya Huduma za simu Vodacom, imesema iko tayari kukutana na Yanga kujadili suala utata wa jezi.

Yanga imesusa kuvaa jezi za kampuni hiyo zenye nembo ya rangi nyekundu, wakidai kufanya hivyo ni kwenda kinyume na katiba ya klabu ambayo haitambui rangi hiyo.

Kauli hiyo ya Vodacom imekuja siku moja baada ya Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga kutaka pande hizo mbili kukaa chini na kufikia muafaka.

Meneja Masoko wa Vodacom, Kelvin Twisa alisema milango iko wazi kwa Yanga kuja kujadili hoja za udhamini kama wanaona kuna kasoro kati yao.

No comments:

Post a Comment