tuwasiliane

Saturday, September 8, 2012

Mourinho aitaka Man City imsahau Ronaldo




KOCHA wa Real Madrid, Jose Mourinho amekiri kwamba Manchester City ambayo imekuwa ikitumia fedha nyingi kwa ajili ya usajili inaweza kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa Ulaya lakini watanakiwa kukumbuka kitu kimoja; 'Kamwe hawawezi kumsajili Cristiano Ronaldo.

Kocha huyo ameongeza kuwa Manchester City inaweza kunyanyasa katika Kundi D lakini haiwezi kununua historia ya klabu kama Real Madrid.

Manchester City itakutana na kikosi cha Mourinho katika mechi ya fungua dimba ya Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumanne wiki ijayo, baada ya kupangwa katika kundi moja sambamba na klabu za Borussia Dortmund na Ajax.

Utata wa mechi hiyo umeongezeka baada ya taarifa kwamba Cristiano Ronaldo anaweza kutua katika klabu ya Manchester City iwapo ataamua kuondoka katika kikosi cha Hispania.

Alipoulizwa iwapo ana wasiwasi wa kumpoteza mchezaji huyo Mourinho alisema: "Tuna fedha za kutosha kumtuliza mchezaji yeyote, vile vile historia ya klabu haionyeshi kwamba kuna wakati huwa inawaruhusu wachezaji wazuri kama Ronaldo."

"Real Madrid, Barcelona na Bayern Munich ni klabu zenye historia kubwa, zina vikombe vya ligi za ndani, vikombe vya Ulaya, na mashabiki wengi, hivyo vyote ni vitu ambavyo huwezi kuvinunua kwa fedha.

"Kila mchezaji mzuri anatamani kuchezea klabu hizo zenye historia kubwa, ambazo zimejaza vikombe katika makabati yao.

Kocha huyo wa zamani wa Chelsea alikiri kwamba uwekezaji wa Sheikh Mansour ni mkubwa, wanaweza kupata ubingwa wa Ulaya na dalili njema ilionekana baada ya Manchester City kupata ubingwa wa Ligi Kuu England msimu uliopita.

Hata hivyo alionya kuwa utaratibu wa Shirikisho la Soka Barani Ulaya (UEFA) wa kusimamia matumizi ya fedha za usajili wa klabu, timu kama Manchester City na Paris Saint-Germain zitabanwa.

"Manchester City ni kikosi chenye nguvu kwa kuwa kina wachezaji wazuri," alisema Mourinho. "Ni timu iliyojengwa kwa ajili ya kupata ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Lakini ni kazi kubwa kumnasa mtu kama Ronaldo kwa kuwa mipango yao haijakaa sawa licha ya kuwa na fedha nyingi."

"Klabu ambayo inaishi kwa kutegemea fedha za mfadhili pekee haiwezi kuwa na nguvu kubwa. Vile vile hawana historia ya maana."

No comments:

Post a Comment