tuwasiliane

Thursday, September 13, 2012

Kocha Azam akosoa ushindi wa Simba


KOCHA wa Azam FC, Boris Bonjuk amesema ushindi wa Simba kwenye Mchezo wa Ngao ya Jamii ulichangiwa kwa asilimia kubwa na mwamuzi aliyechezesha mechi hiyo.

Kwa mwaka wa pili mfululizo, Simba ilitwaa taji hilo baada ya kuifunga Azam FC mabao 3-2, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mechi iliyojaa kila aina ya ushindani.

Kocha Bonjuk alisema mwamuzi Martine Saanya hakusimama kwenye mstari wa sheria 17 za mchezo wa soka na matokeo yake Simba ndiyo iliyonufaika.

"Alishindwa kutafsiri sheria 17 za mchezo wa soka kama zinavyoelekezwa na iko wazi kushindwa kwake kufanya hivyo kuliisaidia Simba," alisema katika hali ya masikitiko.

"Nilishangazwa kuona mwamuzi akitoa penalti kwa Simba. Unaweza kujiuliza, kweli ile ilikuwa penalti halali. Nadhani hakuwa sahihi kabisa," alisema kocha huyo.

Bonjuk alisema wachezaji wake waliondoka mchezoni na kupoteza morali ya kupambana na sababu kubwa ni uamuzi usiozingatia sheria za mchezo wa soka.

Alishangazwa pia kwa kitendo cha kunyimwa adhabu ya penalti waliyostahili baada ya mshambuliaji wake Kipre Tchetche kuangushwa ndani ya eneo la hatari.

"Nassoro Chollo alimchezea vibaya Kipre katika eneo la hatari, lakini mwamuzi akatoa uamuzi tofauti na uliostahili. Aliisaidia Simba kushinda mchezo huo," aliongeza kocha huyo kutoka Serbia.

Aliisifu Simba na kusema ni timu nzuri na inayoundwa na wachezaji wazuri pia.

Tulicheza vizuri kipindi chote cha kwanza na kupata mabao mawili, lakini baada ya mwamuzi kubadilika na kufanya madudu, wachezaji wangu walishindwa kucheza kwa moyo.

Alisema hana uzoefu na waamuzi wa Tanzania, lakini kama huo ndiyo utamaduni wao, basi kuna kila sababu ya kuangaliwa vizuri.

Inasikitisha pale timu zinapojiandaa vizuri halafu zinaishia kuvunjwa nguvu na uchezeshaji mbovu wa waamuzi, aliongeza.

Nina muda mfupi Tanzania, bado naendelea kujifunza mambo mengi, nitafahamu zaidi kuhusu waamuzi kwenye mechi za ligi, alisema zaidi.

No comments:

Post a Comment