tuwasiliane

Wednesday, August 22, 2012

22 AUG.BOCCO AMALIZA MAJARIBIO SUPER SPORT

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, John Raphael Bocco ‘Adebayor’ leo anakamilisha muda wake wa nyongeza wa kufanya majaribio katika klabu ya Super Sport United ya Afrika Kusini.

Katibu wa Azam FC, Nassor Idrisa amekiambia chanzo chetu kwamba, muda wa wiki moja ya ziada ulioombwa na Super Sport kuendelea kumtazama Bocco unamalizika leo na kuanzia jioni wanatarajia kupata taarifa mpya kuhusu mustakabali wa mpachika mabao huyo.

Super Sport ilivutiwa na soka ya Bocco, katika michuano ya Klabu Bingwa ya soka Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, mwezi uliopita, hivyo kumuita kwa majaribio, ambayo akifuzu ataweka historia ya kuwa mchezaji wa pili wa Tanzania kuchezea klabu hiyo, baada ya Suleiman Matola 2005 hadi 2007, akitokea Simba SC.

Katika Kombe la Kagame, Bocco alifunga mabao matano na kushika nafasi ya tatu katika wafungaji bora, nyuma ya Hamisi Kiiza na Said Bahanuzi wa Yanga, aliyeibuka mfungaji bora.

Lakini Bocco pia alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu uliopita, kwa mabao yake 18 akiwapiku hadi washambuliaji wa kigeni waliocheza ligi hiyo msimu huo, Felix Sunzu, Emmanuel Okwi, Kenneth Asamoah, Davies Mwape na Dalington Enyiana.

Tangu aipandishe Ligi Kuu Azam FC msimu wa 2008/2009 kwa mabao yake, akiibuka mfungaji bora wa Ligi Daraja la Kwanza, Bocco amekuwa akiingia kwenye mbio za kuwania kiatu cha dhahabu cha Ligi Kuu, msimu wa kwanza akizidiwa na Boniphace Ambani aliyekuwa Yanga, msimu wa pili Mussa Mgosi aliyekuwa Simba na msimu wa tatu na Mrisho Ngassa, kabla ya msimu uliopita kutimiza ndoto zake za kuwa mfungaji bora wa ligi hiyo.

No comments:

Post a Comment