
MABINGWA wa Ligi Kuu Tanzania Bara timu ya Simba, inashuka dimbani kuvaana na City Stars ya nKenya katika Tamasha la Simba Day litakalofanyika kesho kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange Kaburu, alisema kuwa maandalizi ya tamasha hilo yanaendelea vizuri kama yalivyopangwa.
Kaburu alisema timu hiyo ambayo imeshika nafasi ya nne katika Ligi Kuu, ilitarajia kuwasili jana jioni kwa ajili ya mchezo huo.
Alisema kuwa katika tamasha hilo milango itaanza kufunguliwa saa 4:00 asubuhi, kutokana na shughuli nyingi zitakazofanyika siku hiyo.
Kaburu alisema katika tamasha hilo wachezaji wa zamani watapewa tuzo maalum kwa ajili ya kuthamini mchango wao.
Alisema kuwa licha ya kupewa tuzo kwa wachezaji wa zamani, pia vyombo mbalimbali vitapata zawadi hizo pamoja na waandishi wake.
Kaburu alisema katika tamasha hilo wachezaji wote waliosajiliwa ambao watacheza katika michuano ya Ligi Kuu na michuano ya Kimataifa ambayo Simba itashiriki watatambulishwa siku hiyo.
Alisema miongoni mwa wachezaji hao ni pamoja na mchezaji Mrisho Ngassa, Emmanuel Okwi na mchezaji mwingine ambaye usajili wake umefikia hatua za mwisho atakuwepo katika utambulisho huo.
"Okwi Ngassa ni miongoni mwa wachezaji watakaotambulishwa hiyo kesho hata hivyo kuna mchezaji tumalizia usajili wake atakuwepo kwa ajili ya kutambulishwa, " alisema Kaburu.
Alisema katika tamasha hilo kutakuwa na burudani mbalimbali kama vile ngoma za jadi na bendi ya muziki wa dansi ya Msondo Ngoma.
Kaburu alisema katika tamasha hilo viingilio vitakuwa shilingi, 20,000, kwa VIP A, shilingi 15,000 kwa VIP B na VIP C itakuwa shilingi 10,000.
Katika viti vya bluu vitakuwa shilingi 5000 na viti vya rangi ya chungwa itakuwa shilingi 8000.
Pia Kaburu alisema katika wiki hii maalum klabu ya Simba itakuwa na shughuli mbalimbali na leo wataanza rasmi kutembelea katika Hospitali ya Mwananyamala na kutoa zawadi mbalimbali kwa wagongwa.
Kaburu alisema wakiwa Mwananyamala watatoa vyakula na sabuni na Alhamisi watakwenda kutoa msaada katika kituo cha watoto yatima cha Maunga kilichpo Kinondoni.
Kaburu alisema Ijumaa watamalizia ziara yao kwenye kiwanda cha Bia Tanzania, TBL kama wadhamini wakuu wa klabu hiyo.
No comments:
Post a Comment