tuwasiliane

Tuesday, August 7, 2012

07 AUG. AZAM KUTAMBULISHA KOCHA MPYA


AZAM FC, washindi wa Medali tatu za Fedha, Ligi Kuu msimu uliopita, Kombe la Urafiki na Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, leo wanatarajiwa kumtambulisha kocha wao mpya kutoka Serbia, ambaye atarithi mikoba ya Muingereza Stewart Hall aliyefukuzwa wiki iliyopita.
Habari kutoka ndani ya Azam, zimesema kwamba baada Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya Azam, ambao pia ni mabingwa wa Kombe la Mapindzui, kupitia wasifu wa makocha kibao, walioomba kazi katika klabu hiyo, imeridhishwa na wasifu wa Mserbia huyo.
Mserbia huyo atapewa mkataba wa mwaka mmoja kwa kuanzia na akifanya vizuri ataongezewa mkataba.

Kwa kuajiriwa kocha huyo, Vivek Nagul kutoka India, aliyekuwa anakaimu nafasi ya Stewart, ambaye aliletwa na Muingereza huyo anarejea kwenye majukumu ya kufundisha timu za vijana, wakati Kocha Msaidizi ataendelea kuwa Kali Ongala.
Stewart kabla ya kuja Tanzania mwaka juzi, akianza kufundisha timu ya taifa ya Zanzibar, aliwahi kufanya kazi India kwa miaka miwili.

Akiwa India ndipo alikutana na Vivek na wakafanya naye kazi pamoja na akaridhishwa na utendaji wake, hasa katika eneo la vijana na ndio maana alipotua Azam FC akamleta aje kumsaidia katika eneo hilo.
Vivek amekuwa Kocha Mkuu wa Azam Academy tangu mwaka jana, akisaidiwa na Iddi Cheche na Philipo Alando.

Stewart alifukuzwa Jumatano iliyopita kwa kosa la kukaidi maagizo ya Bodi ya Ukurugenzi ya klabu hiyo, kumpanga Mrisho Khalfan Ngassa katika mechi ya fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame dhidi ya Yanga.

Kikao cha Jumatano hiyo pamoja baina ya Bodi ya Ukurugenzi ya Azam FC, Mwanasheria wa kampuni na kocha Stewart kiliafiki kuvunjwa kwa ndoa hiyo na Azam FC ikawa chini ya Nagul, akisaidiwa na Kali Ongala.

Baada ya mechi ya Nusu Fainali ya Kagame, kati ya Azam na AS Vita ya DRC, Stewart aliitwa na kuambiwa asimtumie tena Ngassa kwa kitendo cha mchezaji huyo kwenda kuibusu na kuivaa jezi ya Yanga, baada ya kufunga bao la ushindi. Ngassa ameuzwa Simba SC, baada ya sakata hilo.
Lakini Stewart katika kikao hicho, kwanza alimtetea Ngassa kutokana na kufunga bao la ushindi na kumuelezea kama mchezaji muhimu kwake, lakini msimamo wa bodi ulikuwa ni asipangwe tena.

Katika fainali, Stewart alimvalisha jezi Ngassa akamuanzishia benchi, lakini kama ilivyokuwa kwenye Nusu Fainali alimuingiza kipindi cha pili timu ikiwa nyuma kwa 1-0 na mwisho wa mchezo ikashinda 2-1 yeye akifunga la pili, dhidi ya Yanga pia alimuingiza timu ikiwa nyuma kwa 1-0.
Lakini Ngassa alishindwa kurudia kile alichofanya kwenye mechi na AS Vita na Yanga ikashinda 2-0.

Mserbia huyo anakuwa kocha wa tano Azam, ndani ya miaka minne tangu ianze kucheza Ligi Kuu, 2008 baada ya Stewart, Mbrazil Neider dos Santos, Sylvester Marsh na Itamar Amorin, Mbrazil mwingine.
Lakini ni Stewart angalau anaacha kumbukumbu ya taji na Medali Azam, baada ya kuiwezesha kutwaa Kombe la Mapinduzi Januari, kushika nafasi ya pili katika Ligi Kuu Aprili, kabla ya kushika nafasi ya pili Kombe la Urafiki na Kagame mwezi uliopita.
Stewart ana sifa ya kutokuwa mbinafsi na mwenye kuwaamini watu wa chini yake, kwa mfano namna ambavyo amekuwa akimpromoti Kali Ongala. Alimkuta Kali kama mchezaji, lakini kwa sababu ya umri kumtupa mkono, akashauriana naye awe Kocha Msaidizi na mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga, akakubali.

Chini ya Stewart, Kali alikuwa akiachiwa timu aiongoze ili kumjengea kujiamini zaidi na mwezi uliopita aliachiwa timu kwenye Kombe la Urafiki, akaifikisha fainali, ambako ilifungwa na Simba kwa penalti kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 90.
Wachezaji wa Azam na makocha wapya wa klabu hiyo, pamoja na baadhi ya maofisa wa klabu hiyo, waliangua vilio, wakati wakimuaga Stewart.

Wachezaji walioongoza kwa kilio Uwanja wa Chamazi Ijumaa iliyopita, ni Luckson Kakolaki, Ibrahim Mwaipopo, Ramadhan Chombo ‘Redondo’, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Hajji Nuhu na Erasto Nyoni, wakati kwa maofisa, aliyeongoza ni Vivek Nagul.
Stewart mwenyewe pia alibubujikwa machozi wakati anaagana na familia yake, aliyoishi nayo kwa zaidi ya mwaka kwa furaha, amani, upendo na mafanikio.

No comments:

Post a Comment