
KOCHA wa Vita Club ya DR Congo, Lusadisu Medard amesema amefurahishwa na viwango vya wachezaji wa Simba, mshambuliaji Felix Sunzu na kipa Juma Kaseja na angependa wajiunge naye katika kikosi chake kinachoshiriki Ligi Kuu ya DR Congo.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Medard alisema wachezaji hao wameonyesha uwezo mkubwa tangu kuanza kwa michuano ya Kombe la Kagame 2012 na kudai kuwa anatamani waichezee Vita.
Alisema pamoja na kwamba Kaseja ni mkongwe, uwezo wake umezidi kuimarika zaidi akiwa langoni huku Sunzu akionyesha kujiamini zaidi kila anapolikaribia lango la mpinzani licha ya kwamba alifunga bao moja tu katika michuano hiyo.
Aliongeza kuwa kosa kubwa wanalolifanya Simba ni baadhi ya wachezaji kutojiamini japokuwa wana timu nzuri.
“Kuna yule mchezaji namba kumi (Sunzu), anacheza vizuri sana akiwa na mpira naona ni jinsi gani anaumiliki kwa ustadi, ni straika mzuri sana, ningependa siku moja acheze kwenye timu yangu. Kaseja uwezo wake pia unaonekana kuongezeka kwa kuwa nilishawahi kumuona kipindi cha nyuma, bado yupo vizuri, hao ndiyo ningependa kuwaona mara kwa mara,” alisema Medard.
No comments:
Post a Comment