BAADHI ya viongozi wa Simba inasemekana ndiyo wanamkwamisha Emmanuel Okwi katika majaribio yake ya Ulaya kutokana na kuvutana kuhusiana na timu ya kumpeleka mfungaji huyo mahiri.
Habari za ndani kutoka ndani ya klabu hiyo, zinaeleza kuwa kuna mgogoro unaofukuta chinichini kutokana na kutunishiana misuli kwa baadhi ya viongozi hao na kusababisha Okwi kukwama.
Makundi hayo mawili kila mmoja lina mapenzi yake katika suala hilo, kila upande ukivuta kamba upande wake na kumweka njia panda nyota huyo.
Makundi hayo ya viongozi inasemekana yamefanya mawasiliano na timu tofauti na kila mmoja anataka kumpeleka Okwi kwenye timu yake.
Kigogo mmoja inadaiwa anataka Okwi aende akafanye majaribio katika timu ya Parma ya Italia ambao ndiyo amekuwa na mawasiliano nayo.
Kitendo hicho inasemekana kinapingwa na kiongozi mwenzake ambaye amefanya dili na Red Bull Salzburg, ambao ni kati ya vigogo vya soka kwenye Ligi Kuu Austria.
Makundi hayo imeripotiwa yana tiketi za timu walizozungumza nazo na kumweka Okwi katika wakati mgumu.
"Unajua imekuwa kama vita ya mafahari wawili kwani nyasi ndiyo zinazoumia (akimaanisha vita ya vigogo hao inamwathiri Okwi)," alisema mtu mmoja aliye karibu na viongozi wa klabu hiyo, ambaye aliomba kuhifadhiwa jina lake.
Hata hivyo, haijaeleweka wazi sababu inayowasukuma viongozi hawa kumng'ang'ania Okwi kwenda kwenye timu wanazotaka wao.
Mganda Okwi hajarudi nchini tangu kumalizika kwa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita ambapo alishika nafasi ya pili kwa kufunga mabao 12.
Pia alitoa mchango mkubwa kuifikisha Simba kwenye raundi ya tatu ya Kombe la Shirikisho.
Katika kuelekea kwenye msimu mpya wa Ligi Kuu Bara, kumekuwa na taarifa nyingi kuhusiana na Okwi ambaye kuna wakati aliripotiwa alikuwa anatakiwa kufanya majaribio katika timu ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini.
Hata hivyo, habari zinadai kuwa Okwi alikuwa Austria kwa ajili ya majaribio hayo.
SOURCE; GAZETI LA MWANASPOTI
No comments:
Post a Comment