

SIMBA leo inashuka dimbani kukamilisha mechi za makundi michuano ya Kombe la Kagame kwa kuivaa Atletico ya Burundi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.Ingawa mchezo huo ni wa kukamilisha ratiba, huku timu zote zikiwa mkononi na tiketi ya kucheza robo fainali, bado upinzani mkali unatarajiwa kuonekana.
Kazi kubwa itakuwa kwa wenyeji Simba wenye deni kubwa kutoka kwa mashabiki wao ambao hawajaridhishwa na kiwango walichoonyesha mpaka sasa.
Baada ya kunyukwa 2-0 katika mchezo wa kwanza dhidi ya URA ya Uganda, na kisha ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya AS Ports, bado mashabiki wa Simba hawajaridhishwa na kiwango.
Mshambuliaji Felix Sunzu alilaumiwa kwa kukosa mabao ya wazi katika pambano dhidi ya Ports, hivyo hakuna shaka kwamba leo atatumia fursa hiyo kurejesha hali ya kuaminiwa na mashabiki wa klabu yake.
Katika pambano hilo, Simba itamkosa beki wake wa kushoto Amir Maftah ambaye ni majeruhi wa kidole cha mkono, huku nafasi yake ikitarajiwa kuzibwa na Kigi Makasi.
"Tumepata pigo kubwa, Amir Maftah ni mchezaji muhimu ambaye ataukosa mchezo. Nafikiri Kigi Makasi anaweza kuziba nafasi yake," alisema Kocha Milovan Cirkovic.
Mbali ya kipute hicho kati ya Simba na Atletico kitakachounguruma majira ya saa 10 jioni, pia kutakuwa na mchezo mwingine wa mapema kati ya Azam itakayoumana na Tusker ya Kenya.
Azam yenye pointi moja pekee kama ilivyo kwa mpinzani wake Tusker, italazimika kuweka masihara pembeni na kupigana kufa na kupona ili kupata ushindi utakaoivusha kucheza hatua ya robo fainali.
Kwa maana nyingine, mshindi katika mchezo huu ataungana na Mafunzo ya Zanzibar ambayo suluhu dhidi ya Tusker ilitosha kuipa pointi mbili na kuiwezesha kutinga hatua ya robo fainali, ikiwa ni baada ya kufungana bao 1-1 na Azam katika mechi ya ufunguzi.
Kocha wa Azam FC, Stewart Hall alikuwa jukwaani akifuatilia mechi ya Mafunzo na Tusker ya Kenya iliyomalizika kwa suluhu na kusema atabadili mfumo kuwabana Wakenya hao na kupata ushindi.
Azam kwa sasa inalazimika kushinda mchezo wake wa kesho dhidi ya Tusker au kutoka sare ya mabao zaidi ya moja kutinga hatua ya robo.
Endapo timu hizo zitatoka sare ya bao moja zitaongezewa muda kumpata mshindi. Azam ina pointi moja sawa na Tusker ya Kenya, wakati Mafunzo ya Zanzabar inaongoza kundi kwa pointi mbili ikiwa imetoka sare ya 1-1 na Azam kisha suluhu na Tusker.
Ni jambo zuri kumfahamu mpinzani wako kabla ya kucheza naye, nilikuja kwa nia moja na angalau nimejua nianzie wapi,î alisema Hall.
ìNi timu nzuri, inaundwa na wachezaji wenye nguvu na maumbo makubwa, nafikiri mchezo utakuwa mgumu wakati wote.î
Stewart alisema atatumia zaidi mawinga na kasi zaidi kufanya mashambulizi kwenye lango la Tusker kwa lengo la kushinda mchezo huo wa kukamilisha hatua ya makundi na kutinga robo fainali.
ìNadhani walinzi wote wa kati ni warefu, tunatakiwa kucheza zaidi mpira wa chini na kasi kupitia pembeni ya uwanja.î alisisitiza kocha huyo.
Azam inaundwa na wachezaji wawili kutoka Kenya ambao ni beki wa kulia Ibrahim Shikanda na winga George Odhiambo 'Blackberry'
No comments:
Post a Comment