tuwasiliane

Saturday, June 23, 2012

23 JUN. GERMAN YATINGA NUSU FAINALI KWA KISHINDO


Ujerumani kwa mara nyingine tena usiku wa Ijumaa, katika uwanja wa PGE Arena, Gdansk, nchini Poland, ilithibitisha kwamba ina uwezo wa kuibuka bingwa wa Euro 2012, wakati ilipofuzu kuingia nusu fainali, kwa mchezo maridadi, ilipoishinda Ugiriki magoli 4-2.

Baada ya ushindi huo wa Wajerumani, sasa kuna uwezekano huenda wakakutana na England katika pambano la nusu fainali.

Ujerumani walipoteza nafasi kadha za kupata mabao, kabla ya nahodha Philipp Lahm, mlinzi, kutoka nyuma na umbali wa yadi 25 akapiga mkwaju safi mno na kuandikisha bao la kwanza katika dakika ya 39, na hata kiongozi wa Ujerumani Angela Merkel akasimama kulishangilia bao hilo.

Kipindi cha kwanza kilikwisha Ujerumani wakiongoza kwa bao hilo moja.

Katika kipindi cha pili, mchezaji wa Ugiriki ambaye huichezea timu ya Celtic ya Uskochi, Georgios Samaras, aliitisha Ujerumani kwa kupata bao la kusawazisha dakika ya 55.

Lakini hayo yalikuwa ni sawa na kuchokora mzinga wa nyuki, kwani Ujerumani, wakitambua kwamba iliwabidi kuinua kiwango chao cha mchezo, na walianza kufunga mabao mfululizo, huku Angela Merkel akisimama na kushangilia kila wakati bao la Ujerumani lilipoingia wavuni.

Sami Khedira aliweza kufunga katika dakika ya 61, na muda mfupi baadaye, Miroslav Klose aliongezea bao la tatu katika dakika ya 68.

Ugiriki wakiwa bado katika hali ya kuchanganyikiwa, walizabwa bao la nne, kupitia mchezaji Marco Reus katika dakika ya 74.

Kinyume na matazamio ya Wagiriki walipopata bao la kusawazisha, sasa walianza kufahamu kulikuwa na uwezo wa kutiwa aibu katika mechi hiyo.

Juhudi zao za kuepuka fedheha ziliwasaidia kidogo, kwani Dimitris Salpingidis aliweza kupata nafasi ya kupiga mkwaju wa penalti katika dakika ya 89, na mechi kumalizika magoli 4-2.

Ujerumani sasa inaisubiri England au Italia katika nusu fainali ya mjini Warsaw, Poland, siku ya Alhamisi.

No comments:

Post a Comment