tuwasiliane

Wednesday, June 6, 2012

06 JUN. MANJI NA MCHAKATO WA UONGOZI WA YANGA


NI KWELI ANATAKA KUIMILIKI YANGA?

*NA KAMA AKIFANIKIWA KUWA MMILIKI ATAIFANYIA NINI YANGA?

*KWANINI BAADHI YA WANACHAMA HAWAMTAKI?


Kwa kipindi kirefu sasa tangu mdanyabiashara maarufu mmiliki wa makampuni yaliyo chini Quality Group of companies Bwana Yusuph ajiingize katika kuidhamini klabu ya Dar Young Africans kumekuwepo na mgawanyiko mkubwa wa kifikra miongoni mwa wanamichezo, wanachama na wapenzi wa Yanga, juu ya madhumuni hasa kabisa ya mfanyabiashara huyo kuisadia Yanga.

Huku baadhi ya watu wakisema Manji ana nia ya dhati kabisa ya kuisadia Yanga na kuifanya kuwa klabu ya kisasa kabisa, na wengine wakibaki kusema kwamba mmiliki huyo wa Quality Group of Companies anataka kuitumia Yanga kibiashara na kujinufaisha binafsi kwa kutumia brand ya Yanga.

Katika kipindi cha awamu mbili za uongozi tofauti pale Yanga, kuanzia wa Wakili Iman Madega mpaka uongozi huu uliopinduliwa wa mwanasheria Lloyd Nchunga, Yusuph Manji amekuwa kitajwa kuhusika na migogoro mikubwa iliyojitokeza ndani ya klabu hiyo.

Hivi karibuni baada ya baadhi ya wanachama wa klabu ya Yanga hasa wakiongozwa na wazee wa klabu hiyo, waliongoza mapinduzi ya kuuondoa uongozi halali wa bwana Lloyd Nchunga, ambaye mara ya kwanza alijaribu kutuna lakini mwishowe akaachia ngazi mwenyewe baada ya kuandamwa sana kiasi cha kuanza kupokea vitisho na kufanyiwa vurugu. Wazee wakachukua timu huku wakitamba wana zaidi ya millioni 750 za kufanya usajili, lakini TFF ikairudisha timu chini ya uongozi wa katibu mkuu Celestine Mwesiga huku wakiagiza ufanyike uchaguzi kama katiba ya klabu inavyosema.

Uchaguzi ukaitishwa kwa mujibu wa kanuni, na kamati ya uchaguzi ikaanza kutoa kutoa fomu za nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Yanga.


Katika hali ya kushtusha siku ya jumatatu mfanyabiashara na mdhamini wa klabu hiyo, Yusuph Manji akachukua fomu ya kugombea uenyekiti wa klabu hiyo yenye maskani yake mitaa ya jangwani, huku akimchukulia mmoja wa wajumbe wa kamati ya usajili Abdallah Ahmed Bin Kleb fomu ya kugombea ujumbe wa kamati ya utendaji, na hatimaye leo Yusuf Mehboob Manji alikuwa mmoja ya wanachama 29 wa Yanga waliorudisha fomu za kugombea nafasi za uongozi mbalimbali ndani ya Yanga.

Kitendo cha Manji kuutaka ubosi wa klabu ya Yanga umeibua hofu na maswali mengi juu ya nia hasa ya mfanyabiashara huyo dhidi ya Yanga, baadhi ya wanachama wa klabu hiyo ambao siku zote wamekuwa wakimpinga Manji kwa namna moja au nyingine wakidai hana nia nzuri ya klabu yao, wameongea exclusively na shaffihdauda.com na kutoa hoja nyingi sana zinazojaribu kuelezea kwanini hawana imani na mpango wa Manji kuwa mwenyekiti wa klabu yao.

1: YUSUPH MANJI VS IMANI MADEGA NA LLOYD NCHUNGA

Wakati wakili Iman Madega anataka kuingia Yanga alikuwa akipigwa tafu kubwa sana na Yusuph Manji mpaka akafanikiwa kuutwa uongozi wa klabu hiyo. Lakini baada ya muda kupita kukatoktokea kutokuelewana baina ya watu hao wawili. Hii ilikuwa ni baada ya Manji kuleta wazo la kutaka Yanga iendeshwe na kampuni. Kwa maana ingeanzishwa kampuni ambayo ingenunua asilimia 51 za Yanga, na asilimia 49 zinazobakia zingekuwa zinamilikiwa na wanachama ambao wangekopeshwa kiasi cha billioni 3 na Manji kwa mkopo wa mwaka mmoja tu, huku akiwawekea sharti kwamba kama wangeshinda kuzilipa billioni 3 zake alizowakopesha ndani ya kipindi walichokubaliana kulipwa na mkopo huo , basi Manji ndio angekuwa mtu wa kwanza kuuziwa hisa zile zile ambazo walishindwa kuzilipia.
Pia katika zile hisa asilimia 51, hakukuwa na sheria zozote za kumkataza mtu yoyote kununua hisa hizo, uwe mwanachama au la ungeweza kununua hisa, hata Manji mwenyewe kama angejisikia kufanya hivyo pia alikuwa na uhuru wa kununua.
Baada ya kuupitia vizuri mpango huo Iman Madega hakuweza kukubaliana na mpango huo kwa hofu, kwamba ule ni mpango ambayo ungeidhuru Yanga.

Baada ya kumshindwa Madega ambaye alifanikiwa kumaliza kipindi chake cha Uongozi, klabu hiyo ikafanya uchaguzi na kupata uongozi mpya chini ya Lloyd Nchunga ambaye naye alipoletewa mpango wa kuanzishwa kwa kampuni na Manji akakataa na matokeo yake timu ikahujumiwa kitu kilichopelekea migomo ya wachezaji, na hivyo timu kufanya vibaya kwenye ligi. Inasemekana baada ya Nchunga kuvimba na kukataa kujiuzulu baada ya kipigo cha 5-0 kutoka watani wao Simba, ndipo bosi Manji alipoanza kutoa mkwanja kwa baadhi ya viongozi na kuwaambia wajiuzulu huku akiwatumia wazee kumtia mshikemshike Nchunga ambaye mwishowe akaamua kujiuzulu na kupelekea kuitishwa kwa uchaguzi mpya.


KIVIPI?

Kiuhalisia tu shilingi billioni 3 ni fedha nyingi sana kwa wanachama wa kawaida wa Yanga ambao ndio wapo wengi kuweza kumudu kuzilipa ndani ya kipindi mwaka mmoja. Hata kama wangemudu kuzilipa basi isingekuwa kirahisi unless kuwe kuna mkono mtu nyuma yao, na kama wangeumudu kwa uwezo wao basi ni wachache sana wangeweza kufanya hivyo, hivyo mwisho wa siku hisa nyingi sana zingerudi mikononi mwa Yusuf Manji.
Huku pia kwenye asilimia 51 za kampuni Manji alikuwa na uhuru wa kununua hisa, hivyo kama Manji akazipata labda asilimia 40 ya hisa alizowalipia wanachama kwa mkopo na wakashindwa kuzilipa na huku kwenye kampuni akanunua japo asilimia 15 tu, kwa maana hiyo angekuwa ndio major shareholder hivyo kumfanya kuwa mmiliki wa Yanga SC.

2: KWANINI HAWATAKI MANJI AIMILIKI YANGA?
Anti-Manji wanasema hawana imani kabisa na Manji kwamba anaitaka Yanga ili kuisadia iwe klabu na yenye mafanikio, bali na kwa maslahi yake binafsi.
Kwanza wanajenga hoja kwamba Manji hakuingia Yanga kwa mapenzi binafsi bali kwa kusukumwa na sababu za kisiasa kwa kuifanya klabu hiyo inayosadikika kuwa na wapenzi wengi zaidi nchini kuwa kichaka cha kujifunikia madhambi yake baada ya kukumbwa na kashfa ya EPA.
Wanasema Manji tofauti na wadhamini wengine waliowahi kuidhamini na kuisadia Yanga kama akina Gulamali na Mohamed Vilani, ambao walikuwa wakiitoa fedha nyingi kuisadia timu yao bila kuidai chochote, lakini Yusuf Manji siku zote amekuwa akiwasainisha kwenye vitabu vya kumbukumbu viongozi kwa niaba ya Yanga kila anapotoa fedha labda ya usajili au kuisadia pale timu inapokwama kiuchumi, na hilo limeshathibitishwa na Manji mwenyewe pale alipokaririwa mara kadhaa akisema anaidai Yanga fedha nyingi bila kuweka wazi ni kiasi gani. Kwa hiyo hawajui ni lini atawadai fedha anazoidai klabu hiyo na kama watashindwa kulipa je atafanya nini?

Anti-Manji wanaendelea kujenga hoja zao kwa kusema kuwa wanahisi kwamba Manji ambaye pia ni mfanyabiashara ambaye anamiliki majengo mengi ya kibiashara hapa nchini anachokihitaji kutoka Yanga kwanza ni kujilipa fedha zote alizotumia kuisaidia klabu hiyo pamoja na zile ambazo zipo nje ya vitabu alizotumia kupata wafuasi waliochini ya himaya yake ndani ya klabu hiyo.

Wanasema wasiwasi wao ni kwamba ikiwa Manji atakuwa mmiliki wa Yanga, ataitumia brand ya klabu hiyo pamoja na assets zake ili kujilimbikizia fedha nyingi kwa kipindi labda cha miaka 3 mpaka mitano na baadae ataliuza tu jina la Yanga ikiwemo timu, na yeye kubaki na assets za Yanga yakiwemo majengo mawili ambayo yote kwenye eneo la kibiashara la kariakoo pamoja na eneo kubwa wanalomiliki Yanga eneo la Jangwani makao makuu ambapo imegundulika Yanga inahodhi eneo kubwa sana ambalo kwa sasa limevamiwa na baadhi ya majirani wanaoishi karibu na makao makuu ya Yanga-Jangwani.

Endapo Manji ataliuza jina la Yanga na kubaki na assets za klabu hiyo kisha kuzitumia kwa matumizi mengine, klabu hiyo itapoteza sehemu ya historia yake kubwa iliyojijengea.


3: ANTI-MANJI WALIVYOPOKEA TAARIFA ZA MANJI KURUDISHA FOMU BILA TEGEMEO LAO IDD KIPINGU KUCHUKUA FOMU.

Baada ya Manji kuchukua fomu za kugombea uenyekiti wa Yanga, kundi la wanachama wanaompinga Manji kwa sababu zao waliamua kutafuta njia za kuweza kupambana nae. Inasemekana wakajaribu kumtumia mtoto wa kigogo wa nchi ambaye nae ana nguvu na ufuasi mkubwa ndani ya klabu hiyo, ili aweze kumshawishi Kanali Iddi Kipingu agombee nafasi hiyo, lakini baada ya Kipingu kushindwa kuhakikishiwa kupewa sapoti ya asilimia 100 ya kuweza kupambana na tajiri Manji akaona bora asijiingize kwenye vita mabayo itaweza kumshushia heshima yake kubwa aliyojijengea kwenye tasnia ya michezo nchini kwa kuangushwa vibaya na Sheikh Mansour wa Tanzania.

1 comment:

  1. utaumia sana ndugu yangu we yanga haikuhusu na wala huusiki nayo, endeleza umbea clouds achana na yanga yetu.

    ReplyDelete