tuwasiliane

Friday, June 1, 2012

01 JUN.Simba waanza kujifua


SIMBA imeanza mazoezi rasmi kwa ajili ya mashindano ya Kombe la Kagame na Ligi Kuu Bara huku klabu za Yanga na Azam FC zikiwa bado hazijaanza.

Mabingwa hao wa Ligi Kuu walianza mazoezi yao juzi hasa wakijiandaa na mashindano ya Kagame yanayotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi wa sita jijini Dar es Salaam.

Simba wameanza kwa kufanya mazoezi GYM iliyopo Chang'ombe jijini Dar es Salaam, ambapo kocha msaidizi wa Simba, Richard Amatre alisema wameanzia huko kwa ajili ya kujiimarisha kistamina zaidi.

"Tumeanza mazoezi tangu jana (juzi) kwa ajili ya maandalizi yetu na mazoezi yanaendelea vizuri,"alisema Amatre ambaye ndiye amebaki na kikosi hicho kwa sababu kocha mkuu wa Simba, Milovan Cirkovic yupo kwao Serbia kwa mapumziko.

"Tumeanza ratiba ya GYM kama ilivyo kawaida, wachezaji wengi walikuwa katika mapumziko baada ya kumaliza mashindano, tunafanya hivi kwa ajili ya kuistua miili yao,"alisema Amatre.

Aliongeza kuwa ratiba hiyo, itaendelea hadi hapo baadaye watakapohamia uwanjani.

Kati ya wachezaji waliokuwapo katika mazoezi hayo mmojawapo alikuwa, Paul Ngalema ambaye alisema,"maandalizi mazuri, kama hivi unavyoona tumeanzia GYM, haya ni mazoezi ambayo yatatuweka katika hali nzuri."

Alisema,"tumeanza vizuri kama unavyoona, naamini mambo yatakuwa mazuri hapo baadaye,"alisema Ngalema aliyesajiliwa kutoka Ruvu Shooting.

Hata hivyo bado baadhi ya wachezaji wa Simba hawajajiunga na mazoezi hayo kwa sababu wengine wapo katika vikosi vya timu zao za Taifa.

No comments:

Post a Comment