tuwasiliane

Wednesday, May 2, 2012

02 MAY. Vyuo vikuu vyatakiwa kufundisha ujasiriamali


VYUO vikuu vya Afrika Mashariki, vimetakiwa kuwapa wanafunzi wao mafunzo ya ujasiriamali na yanayoendana na mahitaji ya soko la ajira la Afrika Mashariki.

Mwenyekiti wa Umoja wa Waajiri Afrika Mashariki, Jacqueline Mugo, alisema hayo jana kwenye uzinduzi rasmi wa umoja huo jijini hapa.

Alisema waajiri wengi katika ukanda wa Afrika Mashariki wanakumbana na changamoto nyingi ikiwamo kutopata wafanyakazi walioiva kwenye maeneo yao ya kazi.

“Hii ni moja tu ya changamoto nyingi tunazokumbana nazo katika utendaji wetu wa kila siku kama waajiri na hivyo tunaamini kupitia mwavuli huu, tutakaa pamoja kama waajiri na wadau wengine kupata suluhisho la matatizo yetu,” alisema Mugo.

Alisema ipo haja kwa vyuo kuja na mkakati mpya wa namna ya kuwaivisha wanafunzi wao kwa kuwapa nyenzo muhimu zitakazofanya wapate ajira kwenye soko la Afrika Mashiriki ambalo lina upinzani mkubwa.

“Wanafunzi wanaomaliza vyuo wanatakiwa kuivishwa vya kutosha kabla ya kuingia kwenye soko la ajira…wana mchango mkubwa katika kuimarisha utangamano wa Afrika Mashariki kutokana na mchango wao katika nchi wanachama.

“Kupitia mwavuli huu, tutaishauri Serikali namna ya kuboresha mambo mbalimbali ili kukuza na kudumisha utangamano wetu,” alifafanua Mugo.

Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri Afrika Mashariki, Musa Sirma, alilipongeza jukwaa la waajiri kwa kuja na mkakati wa namna ya kudumisha utangamano huo.

Sirma ambaye ni Waziri wa Masuala ya Jumuiya wa Afrika Mashariki wa Kenya, alisema jukwaa hilo limekuja wakati mwafaka ambapo Jumuiya inatekeleza Itifaki ya Soko la Pamoja.

Alisema Jumuiya itafanya kila linalowezekana kuhakikisha waajiri wanafanya kazi yao katika mazingira bora na kudumisha utangamano.

No comments:

Post a Comment