tuwasiliane

Tuesday, May 1, 2012

01 MAY. MAWAZIRI WAGONGANA KWA WAGANGA WA KIENYEJI


NaHaruni Sanchawa
WAKATI Rais Jakaya Kikwete (pichani) akijipanga kuunda baraza jipya la mawaziri baada ya kuwasilisha hoja ya kulivunja baraza hilo kwenye Kamati Kuu ya CCM ambayo nayo imeridhia hoja yake, baadhi ya mawaziri wamekuwa wakigongana kwa mganga mmoja wa kienyeji, Mlingotini, Bagamoyo.

Habari ambazo gazeti hili imezipata zinadai kuwa mawaziri watatu wamekuwa wakienda katika kijiji hicho kwa nyakati tofauti na kukutana na mganga huyo wa kienyeji anayetajwa kuwa ni maarufu.

Mtoa habari wetu aliyeomba hifadhi ya jina lake kwa kuwa mmoja wa mawaziri waliokwenda huko wana urafiki alisema nia ya safari yao huko ni kung’arisha nyota na wengine kutaka wasing’olewe.

“Mmoja ameonekana Mlingotini Bagamoyo lakini sijasikia akiguswa na kashfa, inawezekana anataka kung’arisha nyota ili achaguliwe tena wakati Rais Kikwete atakapounda baraza lake upya,” kilisema chanzo.

Mawaziri wawili waliotajwa kuonekana Bagamoyo walipozungumza na gazeti hili walikataa katakata na kudai kuwa waliowataja ni maadui zao wa kisiasa. Hata hivyo, picha zao hazikuweza kupatikana mara moja.

Rais Kikwete analazimika kuvunja baraza la mawaziri baada ya wengi kutuhumiwa bungeni kuwa wamefuja fedha za umma.

Mawaziri hao wametakiwa kujiuzulu baada ya kuwasilishwa kwa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ikionesha ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma uliofanywa na viongozi wa idara za serikali.

Wanaotakiwa kung’oka ambao picha zao zipo ukurasa wa mbele ni Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika, Jumanne Maghembe na Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige.

Wengine ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Cyril Chami, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi),George Mkuchika, Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu na Waziri wa Afya, Dk. Hadji Mponda.

SOURCE; GLOBAL PUBLISHERZ

No comments:

Post a Comment