tuwasiliane

Friday, April 27, 2012

27 APR. JE AZAM GONJWA JINGINE KATIKA SOKA LETU?



Ukipita katika vijiwe vya soka la bongo hukosi stori ama uvumi wa Azam FC kutumia mchezo mchafu ambao unasadikika kutumiwa na vilabu vikongwe Simba na Yanga.

Ndani ya miezi miwili waamuzi wa tatu waliochezesha michezo ya Azam FC wamepigwa huku mpambano wao mmoja dhidi ya Mtibwa Sugar kuvunjika.

Je ni kweli Azam FC wanatumia ukubwa wa mfuko wake kuwaonga waamuzi wa michezo yao, kama hapana ni kwanini kushuhudiwe maamuzi yenye utata katika michezo yake?

Tufunguwe kwa kumsoma mkeleketwa wa Azam FC ambaye pia ni meneja wa Azam FC Patrick Kahemele (PK) kama alivyonukuliwa na blog ya BIN ZUBEIRY;

"Tatizo timu za Tanzania kama walivyo mashabiki wake ni Simba & Yanga, wachezaji, makocha, viongozi hadi mashabiki wao wamekalia uwakala wa kuzisaidia Simba na Yanga.

Kama Azam FC ingekuwa inashika nafasi ya saba (7) ikiwa pointi 15 nyuma ya Simba na Yanga msingesikia refa kupigwa wala nini lakini kwa kuwa kwenye mechi za Azam FC zinaamua nafasi ya Simba/Yanga kwenye ubingwa na uwakilishi wa nchi kimataifa basi unashangaa watu wanakuja kuhakikisha wanaisimamisha Azam FC ili wawafurahishe Simba au Yanga....

Tanzania ni nchi ambayo viongozi wa vilabu vya ligi kuu ni wanachama wa Simba/Yanga tena wanahudhuria mikutano na kupiga kura, ...... hawa watu wanakuja viwanjani na chuki, jazba na unazi.

Tanzania ni nchi ambayo timu zipo tayari kushuka hata daraja lakini wawe wametimiza azma yao ya kuzisaidia Simba/Yanga. ni kipindi cha mpito na kitapita, ndiyo maana tunapigania mpira wetu uwe kwenye TV ili mambo yanayofanyika kila mtu aone. Azam FC haikatishwi tamaa na itaendelea kupambana na dhamira yetu ni kuhakikisha tunaleta kikombe cha Afrika in the next five years.

Waliwatisha na baadaye kuwashusha daraja baadhi ya timu ambazo zilikuwa zinaleta Challenge, wamejaribu kwa Azam FC wameshindwa na hakika hawataweza kamwe. Hii ni nchi ambayo mashabiki wake walishangilia Moro United ya Balhabou kuukosa ubingwa wakati ilikuwa ikiongoza kwa pointi 13 huku ligi ikiwa imebakiza mechi 5 tuu.... leo walitaka Azam FC ifungwe mfululizo ili Simba na Yanga zipate nafasi,

Tunasema tutapambana hadi mwisho wa ligi... na Ubingwa Tunautaka,"mwisho wa nukuu.

Naingiwa na utata kila nikiangalia ndoto ya klabu ya Azam na uvumi huu wa kununua waamuzi, baada ya kutumia mamilioni katika kuhakikisha wanatimu bora. Huenda uvumi huu si kweli na ni vigumu kuukata uvumi huu kwa matukio yanayojiri katika michezo ya Azam FC ambayo ina msingi wa wachezaji ambao wanauwezo wa kuimba uhai kwa muda mrefu.

Ila kama ni kweli Azam FC wanatumia mgongo wa nyuma kupata matokeo ni dhahiri, itakuwa ugonjwa mwingine katika soka la bongo badala ya kuwa tiba.

Kuna namna mbalimbali ya kumshinda mpinzani wako na moja ya njama ni kumpaka sifa mbaya huyo mpinzani wako, huenda hiyo hoja inajengeka kutokana na makosa wanayofanya marefa hutokea katika michezo mingine ya ligi kuu na usikii mwamuzi kupigwa.

Mathalani goli la Aggrey Morise katika mchezo dhidi ya Polisi Dodoma ambapo kabla ya mpira kumfikia mfungaji kunadaiwa kipa wa Polisi alifanyiwa madhambi, kitendo kama hiko kilitokea katika mchezo kati ya Yanga na Villa Squad.

Mchezo kati wa yanga na Azam ndipo falsafa na uvumi huo ulipo pata kasi, na dakika za Mwanzo facebook ya Yanga ilikuwa imeanza kuandika mwamuzi kushindwa kumudu pambano, wakati huo mwamuzi aliyeshutumiwa kuchukua hela kwa Azam akikataa kuwapa Azam penati ambayo wengi wao wangelala katika maamuzi yake, hapo ikiwa kabla ya Niyonzima kupewa kadi nyekundu ambayo kwangu naiita kadi ya kujitakia.

Mchezo wa mwisho dhidi ya Mtibwa Sugar kulijaa utata mtupu na sikushangaa kusikia waamuzi wa mchezo huo wakifungiwa.

Na huo mchezo ndio nilipo ingiwa na imani ya kuanza kuamini uvumi wa Azam kuutumia njia ya mkato kujipatia matokeo, kwa maamuzi yote yenye utata katika mchezo huo kuwa lalia Azam FC. Na kuiona Azam FC ni gonjwa jingine katika soka la bongo.

No comments:

Post a Comment