Wednesday, April 25, 2012
25 APR.Papic azuiwa kuondoka Dar es Salaam
KOCHA Mkuu wa Yanga aliyetangaza kumaliza mkataba wake na klabu hiyo, Kostadin Papic amezuiwa kuondoka jijini Dar es Salaam kurejea kwake kwa vile bado ana mkataba na klabu hiyo.
Kutokana na hali hiyo uongozi wa Yanga umemtaka Papic aendelee kuinoa timu yao mpaka baada ya mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Yanga na Simba Mei 5 mwaka huu ambao utakuwa wa mwisho kufunga msimu wa ligi hiyo mwaka 2011/12.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga alisema Papic hawezi kuondoka kwani mkataba wake na Yanga unamalizika baada ya ligi kwisha tofauti na alivyoeleza yeye.
“Sifahamu kwa nini hili limejitokeza, lakini mkataba upo wazi kwamba ni baada ya ligi kumalizika na ligi itaisha Mei 5, hivyo kuondoka ni kushindwa kufuata mkataba ulivyo.
“Nimezungumza naye leo (jana) kuhusu jambo hili na tumekubaliana, hawezi kuondoka ataiongoza timu kwenye mechi yetu na Simba, mkataba upo hivyo, labda kwa vile ratiba ya ligi imebadilishwa mwanzo ilikuwa imalizike Aprili, pengine ndiyo maana aliutafsiri hivyo,” alisema Nchunga.
Jumapili baada ya mchezo wa Yanga na Polisi Dodoma Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Papic aliwaambia waandishi wa habari kuwa mkataba wake na Yanga umemalizika, hivyo hawezi kuendelea kuinoa timu hiyo na atakapokuwa amemalizana nao baadhi ya madai yake angeondoka kurejea kwao. Papic hakupatikana jana kuzungumzia suala hilo.
Wakati huohuo, mambo yamezidi kuwa magumu ndani ya Yanga baada ya wajumbe wengine wawili wa Kamati ya Utendaji, Abdallah Binkleb na Seif Ahmed kutangaza kujiuzulu nafasi zao.
Taarifa zilizopatikana kutoka kwa wadau wa karibu wa wajumbe hao jana zilieleza kuwa tayari waliandika barua za kujiuzulu na zimeshamfikia Nchunga.
Alipoulizwa kuhusiana na suala hilo, Nchunga alikiri kupata taarifa za kujiuzulu wajumbe hao, lakini akisema kwa sasa hayupo katika nafasi ya kuzungumzia jambo hilo.
Mjumbe mwingine wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Sarah Ramadhan alitangaza kujiuzulu wadhifa wake wiki iliyopita kwa kile alichodai ni kutokana na matokeo mabaya ya Yanga kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, ambapo imeshindwa kushika nafasi mbili za juu.
Wakati huohuo, Kocha Mkuu wa Simba Milovan Cirkovic amesema kikosi chake kitaibuka na ushindi kwenye mechi ya mwisho ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya wapinzani wao wakubwa Yanga.
Akizungumza mara baada ya mechi ya Simba na Moro United kwenye Uwanja wa Taifa juzi ambapo Simba ilishinda mabao 3-0 na kuendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo alisema jinsi timu yake inavyocheza kwa sasa hana shaka itashinda mechi yake hiyo dhidi ya Yanga Mei 5.
Pambano hilo baina ya timu hizo zenye upinzani wa kihistoria hapa nchini ndiyo inatarajia kuamua bingwa wa msimu huu, kwani Simba itahitaji ushindi ama sare ya aina yoyote kuchukua ubingwa huo lakini kama itapoteza mechi hiyo ni wazi kama Azam inayoshika nafasi ya pili ikashinda mechi zake zilizosalia basi itakuwa mabingwa wapya wa ligi hiyo.
Alielezea kufurahishwa kwake na kiwango kinachooneshwa na timu hiyo kwa sasa na kuongeza kuwa kama itaendelea kucheza namna inavyocheza sasa ni wazi itatwaa kombe la ligi msimu huu na Yanga ndiyo itatumika kuwapa ubingwa.
SOURCE HABARI LEO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment