Friday, April 20, 2012
20 APR. KUTOKA TFF
Release No. 061
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Aprili 20, 2012
KOCHA NGORONGORO HEROES AAHIDI USHINDI
Kocha Kim Poulsen anayeinoa timu ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 cha Tanzania (Ngorongoro Heroes) ameahidi kikosi chake kufanya vizuri kwenye mechi dhidi ya Sudan.
Akizungumza jana (Aprili 20 mwaka huu) kwenye mkutano na Waandishi wa Habari, Poulsen amesema timu yake imejiandaa vizuri kwa mechi hiyo na kiu yao ni kushinda.
Kwa upande wake Kocha wa Sudan, Azhari Osman El Tahir amesema ingawa haifahamu vizuri timu ya Tanzania, lakini wamejiandaa kushinda kwani kwa muda mrefu walikuwa hawajashiriki mashindano ya vijana ya kimataifa.
Mechi hiyo ya michuano ya Afrika kwa vijana wenye umri huo itachezwa kesho (Aprili 21 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni kwa viingilio vya sh. 3,000, sh. 5,000, sh. 10,000 na sh. 15,000.
Sudan iliwasili nchini jana (Aprili 19 mwaka huu) ikiwa na kikosi cha wachezaji 20, viongozi kumi na mwandishi wa habari mmoja kwa ajili ya mechi hiyo ya kwanza kabla ya timu hizo kurudiana jijini Khartoum kati ya Mei 4, 5 na 6 mwaka huu.
Mechi hiyo itachezeshwa na mwamuzi Brian Miiro atakayesaidiwa na Mark Ssonko, Lee Patabali na Denis Batte wote kutoka Uganda. Ejigu Ashenafi wa Ethiopia ndiye atakayekuwa Kamishna wa mechi hiyo namba 15.
Fainali za Afrika kwa michuano hiyo zitafanyika Machi mwakani nchini Algeria wakati za Dunia zitafanyika nchini Uturuki kuanzia Juni hadi Julai mwakani. Katika fainali za Dunia, Afrika itawakilishwa na timu nne za kwanza kwenye fainali za Algeria.
MALINZI MGENI RASMI MKUTANO MKUU TFF
Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Dioniz Malinzi anatarajia kuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) utakaofanyika kwa siku mbili (Aprili 21 na 22 mwaka huu) kwenye ukumbi wa NSSF Waterfront jijini Dar es Salaam.
Wajumbe wa mkutano huo watawasili jijini kesho (Aprili 20 mwaka huu) na watafikia kwenye hoteli ya Royal Valentino. Wajumbe wanatoka katika vyama vya mpira wa miguu vya mikoa, vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu ya Vodacom.
Mkutano huo utakaoanza saa 3 asubuhi utakuwa na ajenda kumi na moja. Baadhi ya ajenda hizo ni hotuba ya Rais wa TFF, taarifa ya utendaji ya mwaka 2011, bajeti ya mwaka 2012 na taarifa ya ukaguzi wa hesabu (audited accounts).
MECHI ZA VPL WIKIENDI HII, MAREKEBISHO
Ligi Kuu ya Vodacom inaingia raundi ya 24 wikiendi hii kwa mechi mbili zitakazochezwa Aprili 22 jijini Dar es Salaam. Villa Squad itaumana na African Lyon kwenye Uwanja wa Chamazi wakati Yanga itakuwa mwenyeji wa Polisi Dodoma katika Uwanja wa Taifa.
Azam na Mtibwa Sugar zilizokuwa zicheze Aprili 21 mwaka huu sasa zitacheza Aprili 23 mwaka huu kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam wakati siku hiyo hiyo jioni kutakuwa na mechi kati ya Simba na Moro United. Mechi zote zitaanza saa 10.30 jioni.
Aprili 25 mwaka huu Oljoro JKT itaikaribisha Yanga kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha wakati JKT Ruvu itakuwa mwenyeji wa Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
Raundi ya 25 itakamilika kwa mechi nne; Aprili 28 mwaka huu Coastal Union itakuwa mwenyeji wa Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga huku Mtibwa Sugar ikiwa mgeni wa African Lyon kwenye Uwanja wa Chamazi. Azam na Toto African zitacheza Chamazi, Aprili 30 mwaka huu wakati Mei 1 mwaka huu Villa Squad itaumana na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Chamazi.
Ligi hiyo itafunga msimu wa 2011/2012, Mei 5 mwaka huu ambapo timu zote 14 zitakuwa uwanjani. Simba vs Yanga (Uwanja wa Taifa), Oljoro JKT vs Polisi Dodoma (Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha), Ruvu Shooting vs Villa Squad (Mabatini, Mlandizi), Coastal Union vs Toto African (Mkwakwani, Tanga), African Lyon vs JKT Ruvu (Manungu, Morogoro), Azam vs Kagera Sugar (Chamazi, Dar es Salaam) na Moro United vs Mtibwa Sugar (Jamhuri, Morogoro).
WASWAZI KUCHEZESHA SIMBA, AL AHLY SHANDY
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeteua waamuzi kutoka Swaziland kuchezesha mechi ya kwanza ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho kati ya Simba na Al Ahly Shandy ya Sudan itakayochezwa Aprili 29 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Waamuzi hao wa mechi hiyo namba 71 ni Nhleko Simanga Pritchard atakayepuliza filimbi wakati wasaidizi wake ni Mbingo Petros Mzikayifani na Sibandze Thulani. Mwamuzi wa mezani atakuwa Fakudze Mbongiseni Elliot.
CAF pia imemteua Kayijuga Gaspard wa Rwanda kuwa Kamishna wa mechi hiyo.
KAMPUNI NNE ZAPITA TENDA YA TIKETI
Kampuni nne kati ya sita zimepita hatua ya kwanza ya mchakato wa kupata moja itakayofanya kazi ya kutengeneza tiketi za elektroniki kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom na nyingine zinazosimamiwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Shughuli ya ufunguzi wa maombi ya hatua ya awali ya kuonesha nia (Expression of Interest) kwa ajili ya tenda hiyo ilifanywa jana (Aprili 19 mwaka huu) na Kamati ya Mipango na Fedha ya TFF ambayo ndiyo Bodi ya Tenda ya shirikisho.
Kampuni ambazo zimepita hatua hiyo ya kwanza sasa zinatakiwa kuwasilisha rasmi tenda zao kwa ajili ya shughuli hiyo ndani ya kipindi cha wiki tatu tangu ulipofanyika ufunguzi wa hatua ya kwanza.
Baadaye Bodi ya Tenda itakutana tena kupitia tenda zitakazokuwa zimewasilishwa na kufanya uteuzi wa kampuni moja itakayofanya kazi hiyo.
Kampuni ambazo zimefanikiwa kuingia katika hatua hiyo ya pili ni CRDB Bank PLC, SKIDATA People Access Inc., Prime Time Promotions na Punchlines (T) Limited.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment