tuwasiliane

Thursday, April 19, 2012

19 APR.Chuo Kikuu cha Mandela kitafungua milango ya teknolojia


TANZANIA imefungua ukurasa mpya kisayansi na teknolojia, katika kufungua chuo kikuu cha sayansi na teknolojia cha Mandela.

Chuo Kikuu cha Nelson Mandela, kilichojengwa Tengeru, mkoani Arusha, Tanzania, kimefungua ukurasa mpya katika kufikia malengo ya maendeleo ya sayansi na teknolojia nchini.

Katika kuhakikisha chuo hicho kinaanza kwa kasi inayokusudia, Rais Jakaya Kikwete amemteua Dk. Mohamed Gharib Bilal kuwa Mkuu wa Chuo hicho, ambaye ni kiongozi wa pili kwa madaraka nchini kutoka Rais mwenyewe.

Kwa mujibu wa Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, katika taarifa iliyotolewa na Katibu
Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, Rais Kikwete pia amemteua Profesa David Mwakyusa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho cha Nelson Mandela.

Uteuzi wa Dk. Bilal ambaye ni Makamu wa Rais na Profesa Mwakyusa aliyepata kuwa Waziri wa
Afya na Ustawi wa Jamii katika serikali ya Rais Kikwete, kukamilisha mustakabali wa kuimarisha elimu ya sayansi na teknolojia nchini.

Uteuzi huo uliofanyika Aprili 5, mwaka huu, unakifanya chuo hicho kiwe kimakamilika safu ya uongozi wa juu, akiwamo Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Burton Mwamila.

Chuo cha Nelson Mandela ni moja ya vyuo vikuu vinne, vinavyolenga kuendeleza sayansi na teknolojia katika Bara la Afrika, hadi kukamilika kimetumia zaidi ya Sh bilioni 38, lengo likiwa kutoa elimu bora inayokusudiwa kuwainua Waafrika katika sayansi na teknolojia.

Chuo hicho kilichopo Tengeru wilayani Arumeru mkoani Arusha, kimekamilika na kitaanza kuchukua wanafunzi mara moja, ambao watakuwa wakichukua shahada ya pili na kuendelea juuu.

Profesa Burton Mwamila amesema ujenzi wa chuo hicho, umegharimu Sh bilioni 38, ambazo ni fedha za Serikali ya Tanzania, jambo linalothibitisha nia ya dhati ya serikali kuwa na uwanja
mpana wa elimu ya sayansi nchini.

“Hivi sasa kilichobaki ni kuweka samani na vifaa vya kufundishia maana majengo yote yamekamilika na tutaanza na wanafunzi 92 ambao wamekwisha kudahiliwa na watajiunga
rasmi na chuo mwezi ujao,” anasema Profesa Mwamila.

Profesa Mwamila anasema kuwa wanafunzi wa chuo hicho kwa sasa wanatoka Tanzania, Malawi, Ethiopia na Uganda, lakini pia milango ipo wazi kwa wengine kadiri siku zitakavyokuwa zinasogea.

Katibu Mkuu, Philemon Luhanjo, ambaye sasa ni mstaafu, akiwa na makatibu wakuu wengine kutoka Ikulu, wizara za Ardhi, Maji, Fedha na Ofisi ya Waziri Mkuu, waliwahi kutembelea chuo hicho kipya na kusema kitakuwa bora kuliko kile cha Dodoma.

“Tulianza kujifunza na kile cha Dodoma sasa tunaendelea kujenga vyuo vyenye ubora zaidi na tunatarajia kukitumia hiki cha Mandela kuitangaza Tanzania katika nyanja za kimataifa,” anasema Luhanjo.

Chuo hicho maarufu miongoni mwa vyuo vikuu vinne barani Afrika, chini ya mtandao wa elimu wa Taasisi ya Rais mstaafu wa Afrika Kusini na mpigania uhuru kwa miongo mitatu akiwa jela, Nelson Mandela.

Vyuo vingine katika mtandao huo vinajengwa nchini Afrika Kusini, Nigeria na hiki cha Tanzania ambapo mzee Mandela alisisitiza kuwa chuo cha ukanda wa Mashariki kijengwe jijini
Arusha.

Chuo Kikuu hicho hadi kufikia uwezo wake wa juu kitakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 6,000, ambao ni wengi katika kuinua elimu ya sayansi na teknolojia nchini ambayo ni msingi katika kujenga uchumi wa nchi.

Chuo kikuu hicho pamoja na vyuo vikuu vingine, vinatakiwa kuhakikisha vinatoa mchango muhimu utakaowezesha ukuaji wa uchumi na kuwa na usalama wa chakula hapa nchini.

Balozi Maalumu wa Rais Barack Obama wa Marekani anayesimamia Usalama wa Chakula na
Maendeleo ya Sayansi na Teknolojia katika Bara la Afrika, Profesa Gebisa Ejeta, alipotembelea chuo hicho ametoa mwito.

Balozi huyo aliyefuatana na Rais wa Chuo Kikuu cha Purdue katika Jimbo la Indiana Marekani, France Cordova, ametoa mwito kuwa vyuo vikuu hivyo vina vinatakiwa kujua kuwa vina mchango muhimu katika kutoa majibu kwa jamii vinavyoitumikia.

Ametoa mfano wa Chuo Kikuu cha Purdue, ambacho kina wajibu wa kuhakikisha usalama wa chakula nchini Marekani, akata chuo kikuu cha sayansi na teknolojia cha Mandela kuiga mfano huo.

Ujumbe huo wa balozi wa Marekani ulikuwa nchini, kuona shughuli zinazofanywa na Chuo
Kikuu hicho na kutiliana saini makubaliano ya ushirikiano baina ya vyuo vikuu hivyo viwili kwa kipindi cha miaka 10 ijayo.

“Tumefurahi kuona jitihada zinazofanywa na Serikali ya Tanzania ili kukifanya chuo hiki kiweze kutoa mchango mkubwa si kwa nchi hii tu bali pia kwa bara zima la Afrika,
tumekubaliana kutakuwa na kubadilishana wataalamu na wahitimu mara kwa mara ili kuwajengea uwezo na kukuza ushirikiano baina yetu,” anasema Profesa Ejeta.

Rais wa Chuo cha Purdue, Cordova, ametoa takwimu za wanafunzi kuwa 237 kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika wamehitimu katika chuo hicho na wanafanya kazi katika nchi zao na mashirika mbalimbali ya kimataifa.

Profesa Mwamila amesema, ujio wa wataalamu hao nchini utachochea kasi ya maendeleo katika chuo hicho, kutokana na umaarufu alionao Profesa Ejeta. Mwaka 2009 Profesa Ejeta alitunukiwa tuzo ya juu katika masuala ya Usalama wa Chakula na Rais Obama, tuzo ambayo inampa heshima kuwa ni mpiganiaji wa masuala ya usalama wa chakula duniani.

Profesa Mwamila amesema kwa kushirikiana na chuo hicho wataweza kufikia malengo yao ya kuzalisha rasilimali watu itakayosaidia vyuo vya utafiti nchini kupata watu watakaoweza kuchochea kasi ya ubunifu wa viwanda ili kuondoa umasikini.

Chuo hicho maarufu kitakuwa kikitoa shahada za uzamili na uzamivu, kozi ambazo zitaandaa wataalamu wa kuinua nchi katika fani hiyo nchini na barani Afrika kwa ujumla.

Maendeleo ya sayansi na teknolojia ni muhimu katika kujenga uchumi wa nchi, hivyo kuanzishwa kwa chuo hicho ni sawa na kuleta teknolojia nyumbani, kwani kwa kuwapo chuo hicho nyumbani Watanzania wengi watapata nafasi ya kusoma.

Wasomi wenye shahada za kwanza katika fani za sayansi, wanatakiwa kutumia nafasi hiyo kupata mafunzo ya uzamili na uzamivu katika chuo kikuu hicho, ambacho kipo nchini kwa lengo la kukuza taaluma zao lakini pia kupanua uelewa wao.

Kuwa na wasomi wengi wa sayansi na teknolojia, kutachangia maendeleo ya jamii ya kitanzania, uchumi wa nchi na kuongeza maarifa katika fani hiyo, ambayo ni muhimu katika
kujenga uchumi wa nchi yetu.

No comments:

Post a Comment