Friday, April 13, 2012
13 APR. YANGA KUACHANA NA PAPIC
MABINGWA wa Tanzania, Yanga wapo mbioni kumnasa kocha kutoka Ureno kuja kurithi mikoba ya Mserbia Kostadin Papic anayemaliza mkataba wake wiki ijayo Aprili 18.
Mmoja wa viongozi wa Yanga ambaye hakutaka kuweka hadharani jina lake alisema kuna makocha wawili ambao CV zao zipo mezani mmoja kutoka Ureno na mwingine kutoka Romania, huku wa Ureno akipewa nafasi kubwa ya kuongoza jahazi hilo la Yanga.
Chanzo hicho cha habari kilisema kuwa wameamua kuachana na Papic kwa kile walichodai kuwa hana jipya katika timu yao huku wakimtuhumu kuwasiliana na marafiki wa Simba 'Friends of Simba' kila mara.
"Hatuwezi kumvumilia kocha ambaye mara kwa mara anawasiliana na Friends of Simba, kwanza nidhamu ya wachezaji wetu imeshuka sana tofauti na mwanzo, tunasubiri mkataba wake uishe alipwe chake aondoke," kilidai chanzo hicho.
Alisema,"kwa kifupi ni kwamba tumeshapata CV za makocha wawili mmoja wa Ureno na mwingine wa Romania, tunasubiri mkataba wake uishe tumalizane naye aondoke zake, mechi yake ya mwisho ni mechi ya Kagera Sugar, hawezi kukaa tena benchi wakati mkataba wake utakuwa umeshamalizika."
Kufuatia hali hiyo, katika mechi ya marudiano na mahasimu wao Simba itakayochezwa Mei 5, Mserbia huyo hatakaa katika benchi la Yanga na huenda Mreno akaongoza jahazi.
Zipo taarifa kwamba Papic hajaongozana na timu yake kwenda Mwanza kwa ajili ya mechi yao ya marudiano dhidi ya Toto Afrika kwa kuwa anaumwa ila ni mgomo baridi baada ya kucheleweshewa mshahara wake wa miezi mitatu hata hivyo habari hizo zimepingwa vikali na Katibu Mkuu wa Yanga, Selestine Mwesigwa.
"Papic hadai chochote, kila mwezi tunampa fedha zake, alidai mshahara wa mwezi mmoja tu hapa alipiga kelele, iweje avumilie mshahara wa miezi mitatu? na hilo la mkataba wake muulizeni mwenyewe kama ataendelea au la, mimi siwezi kuuzungumzia mkataba wake wakati bado haujaisha,"alisema Mwesigwa
Hata hivyo, chanzo kingine cha habari kilisema kuwa Yanga ambayo inapokea Sh 26m kila mwezi kutoka kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kama wadhamini wao ipo kwenye matatizo makubwa ya mtikisiko wa uchumi baada ya kulipa fedha nyingi kwa aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo raia wa Uganda, Sam Timbe waliyemfungashia virago mapema mwaka jana huku akiwa na mkataba wa miaka miwili.
Yanga walilazimika kumlipa Timbe mamilioni ya fedha kitu ambacho kimesababisha mpaka leo klabu hiyo kuyumba kiuchumi na mapema mwaka huu wachezaji wa klabu hiyo walitishia kugoma hadi walipwe fedha zao za mishahara huku Papic akitangaza kubwaga manyanga iwapo uongozi hautamalizana na wachezaji na kwamba asilaumiwe kwa matokeo ya uwanjani.
Wakati huo huo; mabingwa hao wamesema mapambano ya kutetea ubingwa msimu huu bado yanaendelea licha ya kuachwa kwa pointi saba na Simba wanaoshikilia usukani wa ligi hiyo.
Yanga wamesema pamoja na kupokonywa pointi tatu bado wana uhakika wa kuutetea ubingwa huo kama ilivyokuwa mwaka jana, ambapo timu hiyo ilifanya mapinduzi katika hatua za mwisho za ligi na kufanikiwa kutwaa kombe hilo.
Katibu Mkuu wa timu ya Yanga, Celestin Mwesigwa alisema jana jijini Dar es Salaam kwamba bado mapambano yanaendelea ili kutetea kombe lao, ambapo mwaka huu watani wao wa Jadi Simba wameonyesha dalili na nia ya kulitwaa mapema.
"Hatuwezi kukata tamaa licha ya kuwa tumenyang'anywa pointi tatu, matumaini ya kutetea ubingwa wetu yapo na hilo linawezekana," alisema Mwesigwa.
Mwesigwa alihoji kama mwaka jana waliweza kutwaa ubingwa huokwanini mwaka huu washindwe?, huku akisisitiza kwamba mechi tano walizobakisha kabla ya kumaliza ligi hiyo ndiyo zitawafanya walitwae kombe hilo kwa mara nyingine tena.
"Ninachoweza kusema ni kwamba mashabiki wetu wasiwe na wasiwasi, tuliachwa kwa pointi nyingi mwaka jana na bado tukachukua kombe iweje tushindwe mwaka huu?," alihoji tena Mwesigwa na kuongeza kuwa bado ligi inaendelea hivyo mashabiki wao wajiandae kucheka na kushuhudia timu yao ikitwaa ubingwa.
Akizungumzia suala la rufaa yao kupinga maamuzi ya Kamati ya Nidhamu kuwapokonya pointi tatu za mechi dhidi ya Costal Union, Mwesigwa alisema suala hilo liko chini ya Kamati hivyo anaichia ili ifanye maamuzi.
"Nimesikia kwenye vyombo vya habari kwamba Kamati itakutana Jumamosi, lakini mimi sijaambiwa chochote juu ya kukutana huko hivyo nasubiri taarifa kutoka kwao, jambo la msingi ni kusubiri maamuzi ya Kamati,"alisema Mwesigwa.
Yanga inashika nafasi ya tatu nyuma ya Simba inayoongoza Ligi Kuu ikifuatiwa na Azam inayoshika nafasi ya pili hadi sasa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment