Monday, April 9, 2012
09 APR.Mwanzo, mwisho wa Steven Kanumba
JK AAHIRISHA SAFARI YA UGHAIBUNI KUMLILIA, KUZIKWA DAR KESHO
Florence Majani na Jackson Odoyo
“AMKA Kanumba, mama amekuja. Amka baba. Unameremeta baba, ndoa yako ya mwisho hii… kwaheri mwanangu,” ni maneno ya Mama Mzazi wa Steven Kanumba, Flora Mtegoa mara baada ya kuwasili nyumbani kwa marehemu Sinza, Dar es Salaam akitokea Bukoba.
Maneno hayo yaliyokuwa yakiambatana na kilio alikuwa akiyatoa huku akichanganya lugha za Kisukuma na Kiswahili alieleza jinsi alivyopata taarifa za msiba, adhuhuri ya Aprili 7.
Mara baada ya kuwasili Sinza, Vatican nyumba ya marehemu Kanumba ilizungukwa na umati wa waombolezaji, waliokuwa ndani walitoka kumpokea na hata wale waliokuwa jirani na eneo hilo walisogea wakitaka kumuona.
Kuwasili kwa mama huyo kuliongeza machungu kwa ndugu, jamaa, wasanii na mashabiki ya msanii huyo nguli kiasi cha baadhi yao kupoteza fahamu.
Kikwete aahirisha safari
Rais Jakaya Kikwete jana aliongoza mamia ya waombolezaji katika msiba wa msanii huyo akisema alilazimika kusitisha safari yake ya nje ya nchi ili kuungana na wananchi wengine katika maombolezo hayo.
“Nimeguswa na msiba huu, nilikuwa nisafiri lakini nimeamua kuja hapa kuwapa pole ndugu na wasanii wote,” alisema Rais.
Kanumba (28), ambaye anatarajiwa kuzikwa kesho katika Makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam alifariki dunia katika mazingira ya kutatanisha na hadi sasa Polisi inachunguza tukio hilo huku ikimshikilia msanii wa kike, Elizabeth Michael (Lulu).
Ndugu wa marehemu, Seth Bosco ambaye ana sura inayoshabihiana kwa karibu Kanumba alisema kauli ya mwisho kuisikia kutoka katika kinywa cha kaka yake huyo ilikuwa ni ‘nisubiri.’
Alisema jioni ya Aprili 6, mwaka huu, marehemu alimwambia angependa watoke kwenda matembezini pamoja.
“Ilipofika sita za usiku, nilimwambia kuwa mimi nimekwishajiandaa, akasema ‘nisubiri’ na kisha akaingia chumbani mwake,” alisema Seth na kuongeza:
“Kanumba akiwa chumbani kwake, aliingia binti mmoja, ambaye ninamfahamu kuwa ni mtu wake wa karibu. Kwa kuwa namfahamu, sikushangazwa na ujio wake, aliingia chumbani kwa Kanumba.”
Seth alisema baada ya muda, alisikia sauti zilizoonyesha mgogoro wa aina fulani kutoka chumbani humo na alipotaka kuingia, mlango ulikuwa umefungwa kwa funguo.
“Nilisikia Kanumba akimwambia Lulu; ‘Yaani unapigiwa simu na mwanamume wako mbele yangu?’ Baada ya dakika kadhaa za mzozo chumbani, Lulu alitoka akisema kuwa Kanumba ameanguka,” alisema Seth.
Alisema ripoti ya awali ya daktari inaonyesha kuwa marehemu hana jeraha lolote katika mwili wake… “Kama alisukumwa ukutani, basi lazima jeraha lingeonekana katika ubongo, lakini ripoti inaonyesha hana jeraha na mimi nilimkuta marehemu akiwa anatokwa na povu mdomoni, macho yamemtoka, huku akikoroma, cha ajabu hakutokwa damu… bado tunasubiri uchunguzi zaidi wa polisi.”
Akizungumzia msiba huo dada wa marehemu, Kabela Kajumulo alisema: “Ninachoweza kusema ni kuwa, tumepata pengo lisiloweza kuzibika.”
Wasanii wamwelezea
Wasanii wa filamu na muziki waliokuwa katika msiba huo walimwelezea marehemu Kanumba kwamba alikuwa ni mtu wa watu.
Akimzungumzia marehemu Kanumba, mmoja wa wasanii hao, Blandina Chagula (Johari), alisema alikuwa zaidi ya rafiki kwake akisema hawakujuana katika maigizo tu, bali walicheza pamoja tangu utotoni.
“Nimesoma na Kanumba Mwanza, Shule ya Msingi Bugoyi, lakini si hivyo tu, bali mama yake Kanumba na mama yangu ni marafiki wa karibu. Tulikutana tena hapa jijini, lakini yeye akisoma Shule ya Jitegemee mimi, shule nyingine, ndipo tulipojiunga katika maigizo katika Kikundi cha Kaole.”
Johari alisema amepata pigo kwa kuondokewa na Kanumba kwani alikuwa ni zaidi ya kaka na zaidi ya rafiki akisema alikuwa mshauri na alimuonya pale alipokosea.
Alitaja mambo matatu ambayo angependa wasanii wengine wamuige Kanumba. Aliyataja kuwa ni uchapakazi, kujihifadhi na ustaarabu…“Hana mfano wake, alikuwa ni mstaarabu, mwenye upendo na anayejiheshimu,” alisema Chagula.
Ruth Suka (Mainda) ambaye aliwahi kufanya kazi na marehemu Kanumba pia alimwelezea kuwa alikuwa miongoni mwa watu wachapakazi na wanaojiheshimu.
Alisema Kanumba alikuwa kijana mstaarabu na kabla hajawa maarufu, alikuwa akiogopa mno kuwa karibu na wanawake… “Ni mtu aliyejisitiri mno na mambo yake, lakini mazingira yake ya usanii yalimfanya aanze kuchangamka na kujichanganya na watu wa rika zote. Kwa kifupi ni mtu wa kanisa.”
Msanii mwingine ambaye pia alisoma na marehemu Jitegemee, Emmanuel Myamba alisema alikuwa na uhusiano wa karibu na kwamba alifahamu mambo mengi na kujifunza mwengi kupitia kwa marehemu.
Ujumbe wa mwisho
Aprili, 6 mwaka huu Kanumba alitoa ujumbe ulioonekana kutabiri kifo chake, akiyanukuu maneno ya Mwanafalsafa, Albert Pine yaliyosema:
“Tunachofanya kwa ajili yetu tunakufa nacho. Lakini tunachofanya kwa wengine na kwa ulimwengu, kinadumu na ni cha milele.”
WASIFU:
Kuzaliwa: Agosti 12, 1984.
Elimu: Shule ya Msingi Bugoyi, Shinyanga, Shule ya Sekondari Bugoyi, Dar es Salaam Christian Seminary na
mwaka 2004; Shule ya Sekondari ya Jitegemee.
Filamu ya kwanza: Johari njia Panda.
Hadi sasa amecheza filamu zaidi ya 40 ndani na nje ya nchi.
Filamu ya mwisho: Ilikuwa mbioni kuingia sokoni mwezi huu Ndoa Yangu.
SOURCE MWANANCHI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment