tuwasiliane

Sunday, April 8, 2012

08 APR. CHELSEA SAFII



Matumaini ya Tottenham ya kumaliza katika timu nne bora za Ligi Kuu ya kandanda ya England, yamesalia katika halim ya vuta nikuvute baada ya kutoka sare ya bila kufungana na Sunderland.
Katika hali ya kawaida, pointi moja kwa kikosi cha Martin O'Neill ni afueni, lakini kwa Tottenham wenye kuwania Ubingwa wa Ulaya msimu ujao yameingia doa kidogo.

Spurs walianza mchezo vizuri, lakini Sunderland wakicheza kwao walifanikiwa kuwazuia na nafasi za kufunga zikawa haba.

Nafasi muhimu kwao ilikuwa ni pale Rafael van der Vaart, ambaye mikwaju yake miwili iliishia miguuni mwa walinzi wa Sunderland.

Juan Mata alifunga bao la pili la ushindi katika dakika za nyongeza kabla mpira kumalizika na Chelsea wakafanikiwa kuwazamisha Wigan wanaotapatapa wasishuke daraja na kuinua matumaini ya Chelsea kumaliza katika nafasi nne bora za juu.

Branislav Ivanovic akionekana dhahiri ameotea alifunga bao la kwanza la Chelsea katika hali iliyokuwa ya utata baada ya mpira wa juu kutoka kwa Raul Meireles.

Mohamed Diame akionekana kuipatia Wigan pointi moja wakati alipofunga bao la kusawazisha, lakini Chelsea walifanikiwa kuibuka washindi kupitia kwa Juan Mata baada ya mkwaju wa Fernando Torres kugonga mwamba na kurejea uwanjani.

Liverpool ilimaliza hali mbaya ya kupoteza mechi tatu mfululizo wakati walipolazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya Aston Villa ambao wanapigana kuhakikisha wanaepuka kukaa eneo la kushuka daraja.

Villa walikuwa wa kwanza kupata bao baada ya Chris Herd kuachia mkwaju wa pembeni alipopokea pasi kutoka kwa Barry Bannan.

Luis Suarez alidai mikwaju miwili ya penalti ambayo ilikataliwa na mwamuzi kabla Dirk Kuyt kumtengea pasi nzuri Suarez na kupachika bao la kusawazisha.

Bao la Suarez la kichwa liligonga mwamba kabla hatimaye kutumbukia wavuni.

Mabao mawili yaliyopachikwa na Clint Dempsey yaliisaidia Fulham kupata mafanikio machache ugenini msimu huu na pia kumaliza mbio za ushindi mfululizo wa Bolton ambao wamo katika tishio la kushuka daraja.

Fulham walimiliki zaidi kipindi cha kwanza na Dempsey alifungua mlango wa Bolton kwa mkwaju wa yadi 30 wa free-kick.

Dempsey aliongeza bao la pili muda mfupi kabla ya mapumziko baada ya kuunganisha mkwaju wa pembeni wa Damien Duff.

Fulham walijihakikishia ushindi baada ya pande la pembeni la John Arne Riise kutumbukizwa wavuni na Mahamadou Diarra akiwa mita nane tu.

Norwich City wakiwa wameshafungwa mara mbili, walifanikiwa kuwazuia Everton katika pambano lililokuwa la kusisimua kwenye uwanja wa Carrow Road.

Everton walikuwa wa kwanza kupachika bao wakati Nikica Jelavic alipoutumbukiza mpira wavuni uliotokana na pasi ya Phil Jagielka, lakini Jonny Howson akafanikiwa kuisawazishia Norwich.

Jelavic kwa mara nyingine aliifungia Everton kutokana na pasi ya Steven Pienaar.

Lakini Grant Holt alihakikisha hawapotezi mchezo uwanja wa nyumbani baada ya kutumbukiza mpira akiwa karibu na lango la Everton.

West Brom wameshinda kwa mara ya kwanza baada ya mechi tano zilizopita na kuilazimisha Blackburn kupoteza mechi ya tatu mfululizo na zaidi kusogezwa katika lindi la kuteremka daraja.

Martin Ollson alijifunga mwenyewe baada ya Gareth McAuley wa West Brom kupiga mpira wa kichwa akichonga krosi ya Chris Brunt.

Kazi nzuri aliyoifanya mlinda mlango Ben Foster alifanya matokeo yawe hivyo kabla Marc Antoine-Fortune kufunga bao la pili.

Liam Ridgewell alitumbukiza mpira kwa kichwa kutokana na mkwaju wa free-kick wa Graham Dorrans na baadae Anthony Modeste wa Blackburn kutolewa nje kwa kadi nyekundu.

No comments:

Post a Comment