tuwasiliane

Saturday, April 7, 2012

07 APR.Samatta kufanya majaribio Benfica


MSHAMBULIAJI wa zamani wa Simba ambaye hivi sasa anachezea TP Mazembe ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo (DRC), Mbwana Samatta anatarajiwa kwenda nchini Ureno baadaye mwaka huu kwa ajili ya kufanya majaribio katika timu ya Benfica.

Taarifa hizo za kuhitajiwa kwa Samatta na klabu hiyo ya Benfica ambayo katikati ya wiki hii ilitolewa hatua ya robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Chelsea, ilitolewa jana na aliyewahi kuwa Kocha Mkuu wa African Lyon, Eduardo Almeida.

Almeida, ambaye ni raia wa Ureno aliwasili nchini jana kwa ziara ya wiki moja yenye lengo la kusaka na kuibua vipaji vya mchezo wa soka hapa nchini ili wapate nafasi ya kucheza soka la kulipwa barani Ulaya.

Alieleza kuwa maelezo zaidi kuhusiana na mshambuliaji huyo kwenda kufanya majaribio Benfica atayatoa leo atakapokutana na waandishi wa habari.

Kocha huyo aliyebobea katika kufundisha soka la vijana amekuja kumalizia kazi ya kusaka na kuibua vipaji vya soka hapa nchini aliyoiacha miaka mitatu iliyopita, wakati alipokuwa akiifundisha Lyon, chini ya usimamizi wa kituo cha kukuza na kuendeleza michezo cha Jack
Academy kilichopo Mbagala jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia ujio wake mara baada ya kuwasili Dar es Salaam jana, Almeida alisema amekuja nchini kwa lengo la kutafuta vipaji na atashirikiana kikamilifu na wenyeji wake ili kuhakikisha milango inafunguka kwa Watanzania kwenda nje kucheza soka la kimataifa.

Kwa upande wake Jamal Kisongo ambaye ni Mkurugenzi wa kituo cha Jack, alisema hii ni nafasi nyingine kwa vijana wa Tanzania wanaochipukia katika mchezo wa soka kuonesha uwezo ili waweze kupata fursa ya kwenda kucheza soka la kimataifa barani Ulaya.

Kocha Almeida amewahi kuzifundisha timu mbali mbali za vijana za Ureno ikiwemo timu ya vijana wa chini ya umri wa miaka 17 ya Benfica na hivi karibuni amemaliza mkataba wa kuifundisha timu ya soka ya Naval inayoshiriki ligi kuu nchini Ureno.

Samatta hivi sasa anang’ara na TP Mazembe aliyojiunga nayo Juni mwaka jana akitokea Simba, ambayo alichezea msimu mmoja akitokea African Lyon aliyoshiriki kuipandisha kutoka ligi daraja la kwanza hadi Ligi Kuu.

African Lyon ilikuwa ikijulikana kama Mbagala Market wakati ikiwa daraja la chini.

SOURCE HABARI LEO

No comments:

Post a Comment