
KOCHA wa Simba Mserbia Milovan Cirkovic amesisitiza kuwa hahofii kitu chochote wakati huu ambao kikosi chake kiko katika maandalizi ya kuivaa timu ES Setif ya Algeria katika mchezo wao wa raundi ya kwanza ya michuano ya Kombe la Shirikisho utakaofanyika Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Cirkovic alibainisha hayo jana jijini Dar es Salaam huku akisifia wapinzani wake ambao hivi sasa ndio wanaongoza Ligi ya Algeria akisema ni timu nzuri na imara ingawa anabainisha kuwa anatarajia kikosi chake kupata matokeo mazuri katika mchezo huo ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu katika raundi ijayo wakati watakapokwenda kucheza mchezo wa marudiano huko Algeria.
Akizungumzia zaidi kuhusiana na mchezo huo, kocha huyo wa Simba alisema kuwa anauchukulia kama mchezo mwingine wowote ule pamoja na kukiri kuwa Setif ni timu nzuri ingawa anasema kuwa haiogopi kwa lolote na atafanya kila awezalo kuhakikisha kuwa kikosi
chake kinapata matokeo mazuri kwani suala hilo ni muhimu mno.
Aidha Cirkovic alisema kuwa kikosi chake kitaingia uwanjani kwa lengo la kupata ushindi pamoja na kutambua kuwa Algeria wana historia nzuri katika soka la Afrika kwahiyo Setif itakuwa ni timu ngumu lakini atahakikisha lengo la kupata ushindi litafikiwa.
Kwa upande wa maandalizi Kocha Cirkovic alisema maandalizi si tofauti na yale waliyofanya wakati wakijiandaa kuivaa Kiyovu Sport ambapo pia alisema mchezo wa ligi baina ya timu yake na Mtibwa ulikuwa ni mchezo mgumu na mzuri kwa kikosi chake ambao pia ulitumika
kama sehemu ya maandalizi ya mchezo wao wa Jumapili.
Akielezea namna anavyowafahamu wapinzani wao (Setif) , Cirkovic alisema ameona baadhi ya video za mechi za wapinzani wao hao ambazo walicheza zamani mojawapo ya mechi hizo ni ule waliocheza dhidi ya Al Herrach ambao waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 lakini pamoja na kuona mechi zao za zamani na si za hivi karibuni kocha huyo wa Simba anabainisha kuwa kikosi cha wapinzani wao kinaonekana ni imara mno.
Akigeukia maandalizi ya kikosi chake Cirkovic alisema kuwa kikosi chake kinakabiliwa na majeruhi ambao ni Saidi Nassoro ‘Chollo’ pamoja na Mwinyi Kazimoto ambao hawajafanya mazoezi kwa muda sasa hivyo hawako fiti kwa ajili ya kuikabili Setif.
Tayari viingilio vya mchezo huo vimetangazwa ambavyo ni Sh 5,000 kwa viti vya kijani na bluu Sh 10,000 viti vya rangi ya chungwa. Sh 15,000 VIP C, Sh 20,000 VIP B na Sh 25,000 VIP A.
Tiketi zitaanza kuuzwa kuanzia kesho katika vituo vya Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko, Big Bon Kariakoo, Zizou Fashion Sinza na Kijitonyama, Robby One Fashion Kinondoni Studio, Uwanja wa Taifa, Dar Live Mbagala Zakheem na Gongo la Mboto kwenye duka la Michael Maluwe.
Wakati huohuo Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imeiruhusu Simba kutumia Uwanja wa Taifa kwa mazoezi mpaka Ijumaa.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga Serikali imetoa ruksa kwa Simba kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Taifa kwa siku zilizobakia kabla ya mchezo ingawa mazoezi hayo hayaruhusiwi kuhudhuriwa na mashabiki na kutokana na suala hilo uongozi wa klabu hiyo umewaomba mashabiki wa klabu hiyo kutofika uwanjani kushuhudia maandalizi ya vijana wao.
No comments:
Post a Comment