tuwasiliane

Friday, March 23, 2012

23 MARCH. Nyota wa kimataifa kulipwa fidia- Fifa

SHIRIKISHO la Soka la Kimataifa (Fifa) limeahidi kuwalipia bima wachezaji wa timu za Taifa wanaposafiri kwenda kuzichezea nchi zao.

Utaratibu huo ulitangazwa jana na Rais wa Fifa, Sepp Blatter katika mkutano wa mwaka wa Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa) unaofanyika mjini Istanbul na kuongeza kuwa uamuzi huo umetokana na madai ya klabu maarufu za Ulaya.

Klabu hizo zimekuwa zikidai kupata hasara kwa wachezaji wao wanaosafiri nje kwa ajili ya mechi za kimataifa zinazotambuliwa na Fifa.

Hata hivyo, Blatter alisema bima hiyo itaanza kulipwa baada ya vyama wanachama wake kuridhia katika mkutano wao mwezi Mei.

“Hii ni bima kwa wachezaji hao, italipwa kwa klabu na pia vyama vya soka” kwa ajili ya mechi zinazotambuliwa na Fifa kwa mujibu wa kalenda," alisema Blatter mbele ya wajumbe wa vyama 53 vya soka barani Ulaya.

“Tunazingatia maslahi ya wachezaji hao.”

Uamuzi huo wa Fifa unafuatia ule wa Uefa, shirikisho ambalo lilieleza mwezi Januari kwamba kwamba litaweka bima kwa wachezaji wote watakaoshiriki mashindano ya Euro 2012, Juni mwaka huu.

Umoja wa Klabu za Ulaya (ECA) umekuwa ukipigania kuanzishwa kwa mfumo huo.

Umoja huo wenye wanachama 200 ulianzisha shinikizo hilo baada ya klabu ya Bayern Munich ya Ujerumani kumkosa winga Arjen Robben kwa miezi baada ya kuumia wakati akiichezea Uholanzi wakati wa Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010 nchini Afrika Kusini.

Mwenyekiti wa Bayern, Karl-Heinz Rummenigge ambaye pia anaiongoza ECA, alilalamika wakati ule kwamba Robben alirejea akiwa majeruhi na kuwagharimu kiasi kikubwa cha fedha kumtibia.

Rummenigge aliiomba Fifa kuangalia uwezekano wa kuweka bima kwa ajili ya wachezaji wote kutoka akiba yake na mapato kutoka fainali za Kombe la Dunia.

Klabu mbalimbali ambazo zilitoa wachezaji walioshiriki fainali hizo zilinufaika na dola 40 milioni kwa kila mchezaji kwa timu zote 32 zilizoshiriki michuano hiyo.

Licha ya kiasi hicho, Rummenigge alisema Bayern ilipata kiasi cha dola 73,000 pungufu kama malipo ya matibabu ya Robben kwa muda aliokuwa Afrika Kusini.

Blatter alisema jana kuwa mfumo mpya wa bima utaweza pia kutumika kwa mechi za kufuzu kushiriki fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014 kwa klabu za Ulaya, mechi zinazoanza Septemba.

Rais wa Uefa, Michael Platini na uongozi wa ECA waliwahi kukubali kutoa pauni 55 m ( dola 72 m) kwa klabu zote duniani ambazo wachezaji wake watachaguliwa kushiriki mashindano hayo ya nchi 16 watakaoshiriki fainali hizo nchini Poland na Ukraine.

Klabu pia zinaweza kunufaika na bonasi ya dola 70 milioni kama fidia kwa kuruhusu wachezaji wao kushiriki fainali zijazo za Kombe la Dunia nchini Brazil mwaka 2014.

Fifa inatarajiwa kujadili mpango huo mwezi huu katika Kamati yake ya Utendaji mjini Zurich, Uswisi.

No comments:

Post a Comment