
UONGOZI wa Wekundu wa Msimbazi, Simba ya jijini Dar es Salaam, umesema hauna haja ya kwenda kuweka kambi nje ya nchi kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wao wa raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho (CAF), dhidi ya ES Setif ya Algeria.
Simba, imetinga hatua hiyo baada ya kuisukumiza nje ya michuano, Kiyovu Sport ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2, hivyo itakwaana na Wa-Algeria hao mwishoni mwa wiki ijayo.
Akizungumza kwa njia ya simu jana, Mwenyekiti wa Simba, Alhaj Ismail Aden Rage, alisema kwamba, wameona hakuna haja ya kwenda kujinoa nje ya nchi, kutokana na hali ya hewa ya Algeria kuwa sawa na ya hapa nchini.
Rage alisema, pamoja na hali ya hewa, wamebaini kuwa, wapinzani wao si timu ya kutisha sana, hivyo wameona waendelee kujinoa hapa nchini, kupitia michezo ya Ligi Kuu bara inayoendelea kwa sasa.
“Maandalizi ya Algeria yanakwenda vema, ingawa hayatupi presha kubwa sana kwa kuwa tumeshazipata taarifa zao kwa kiasi kikubwa na mwalimu anazifanyia kazi...lakini suala la kambi litaendelea kuwa hapa nchini na huko tutaenda siku chache kabla ya mchezo,” alisema Rage.
Wakati huo huo, WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kati ya Simba na ES Setif ya Algeria Jumapili ya wiki ijayo.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Rage alisema jana kuwa maandalizi kuhusiana na mchezo huo utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam yanaenda vizuri na kwamba vijana wake wanaendelea kujipanga kuhakikisha wanawapa raha Watanzania.
“Simba ndiyo roho ya Tanzania kwa sasa kwa ngazi ya klabu, tunahitaji ushirikiano wa hali ya juu na wadau wote wa soka, bila kujali tofauti ya klabu zetu, naomba sote tuungane kuhakikisha Simba inasonga mbele,” alisema Rage na kuongeza kuwa anashukuru Waziri Sitta amekubali kuwa mgeni rasmi katika mchezo huo na kusema kuwa ES Setif inatarajiwa kuwasili Dar es Salaam Machi 21.
No comments:
Post a Comment