tuwasiliane

Tuesday, March 13, 2012

13 MARCH. YANGA YAMKATIA RUFAA MWAMUZI


UONGOZI wa Klabu ya Yanga, umewasilisha malalamiko yao Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kupinga maamuzi ya mwamuzi, Israel Nkongo, wakati wa mchezo wao dhidi ya Azam FC, uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki.

Akizungumza jijini Dar es Salam jana, Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu, alisema kuwa wamewasilisha rufaa hiyo ndani ya saa 24 ambapo wanaamini itasikilizwa na kufanyiwa kazi.

Sendeu alisema kwa ujumla Yanga haikufurahishwa na baadhi ya maamuzi ya Nkongo, ambayo yalionekana wazi yalikuwa ya upande mmoja.

Alisema wanaamini kamati itakaa na kutoa maamuzi ya haki ambayo yatazitendea haki pande zote.

“Sisi tumeona tuna kila sababu za kukata rufaa ndani ya masaa 24...lengo ni kupinga maamuzi yale, kwani moja kwa moja yalikuwa yakionyesha yanalenga nini, tunajua kamati itakaa na kupitia kwa kina sababu zetu za kukata rufaa ya kupinga maamuzi ya mchezo huo,” alisema Sendeu.

Katika mchezo huo, uliyopigwa Jumamosi iliyopita, Yanga walikubali kipigo cha mabao 3-1, huku nyota wake Haruna Niyonzima na Nadir Haroub 'Canavaro’ wakilimwa kadi nyekundu.

Wakati huo huo uongozi wa yanga wamekanusha taarifa zilizoenea ya kwamba wachezaji wa yanga walimpiga mtoto na kusababisha kifo chake wakiwa njiani wakirejea Kambini.
imewekwa na aboodmsuni at 00:43 0

No comments:

Post a Comment