tuwasiliane

Sunday, March 11, 2012

11 MARCH. MKAMBA RANGERS,MPEPO F.C ZAFANYA VIZURI LIGI YA MKOA MOROGORO


TIMU ya soka ya Mkamba Rangers ya Wilaya Kilombero, Morogoro, imefanikiwa kutwaa
ubingwa wa Mkoa ikiwa ni timu ya kwanza kutoka nje ya Manispaa ya Morogoro kuweza kunyakua taji hilo.

Mkamba Rangers imetwaa taji hilo baada ya kujikusanyia pointi 11 sawa na timu ya Mpepo ya
Kilosa , lakini ikinufaika kwa mabao ya kufunga na kufungwa katika mashindano ya Ligi ya Taifa
ngazi ya Mkoa wa Morogoro.

Timu hiyo imemaliza fainali za ligi hiyo licha ya kupata pointi hizo, imefunga mabao saba na kufungwa mawili, wakati Mpepo ya Kilosa imemaliza pamoja na kupata pointi sawa na kulingana kwa mabao ya kufunga, lakini imefungwa bao tatu.

Akizugumza kabla ya kuwakabidhi zawadi na kikombe mabingwa wapya hao, Mwenyekiti wa Chama cha soka Mkoa wa Morogoro ( MRFA) Pascal Kianga, alizipongeza timu zote zilizoshiriki
ligi hiyo kuanzia ngazi ya makundi hadi hatua ya fainali iliyoshirikisha timu sita, na michuano hiyo kufanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri wa mjini hapa.

“Kwanza nawapongeza washindi ambao ni mabingwa wa soka wapya wa Mkoa na pia washindi wa pili timu ya Mpepo ya Kilosa…naweza kusema mwaka huu viwango vya timu kutoka nje ya Manispaa ya Morogoro vimekua ndiyo maana leo tumeshuhudia timu mbili zikicheza fainali kutoka Wilaya ya Kilosa na Kilombero” alisema Kianga.

Mwenyekiti huyo wa MRFA , mbali na kuwakabidhi mabingwa wapya kikombe, seti ya jezi, mpira na soksi , pia waliwakabidhi zawadi maalumu ya fedha taslimu Sh 100,000 , na washidi wa pili kupewa kifuta jasho cha Sh: 50,000.

Katika mchezo huo wa fainali Mkamba Rangers ilitoa sare ya kufungana bao 1-1 na Mpepo FC , na matokeo hayo yaliiwezesha kunyakua ubingwa huo uliokuwa ukishikiliwa na timu ya Tumbaku (TLTC) ambapo uongozi wa Kampuni hiyo uliamua timu yake isishiriki mashindano hayo mwaka huu.

Hata hivyo matokeo hayo yalichangiwa na timu ya Uhuru Rangers ya mjini Morogoro
kupokwa pointi tatu baada ya wachezaji wake kumpiga mwamuzi wa mchezo wao dhidi ya
Mkamba Rangers na kusababisha mchezo wao kuvunjika katika dakika ya 72 wakati zikiwa zimefungana bao 1-1.

No comments:

Post a Comment