tuwasiliane

Friday, March 9, 2012

09 MARCH.Mikoa mipya 4 na wilaya zake 19 sasa rasmi


SERIKALI imetoa matangazo rasmi ya Serikali kuhusu uanzishaji wa mikoa mipya minne na wilaya mpya 19 ambayo yamechapishwa tangu Machi 2, mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu jana kwa vyombo vya habari, Waziri Mkuu Mizengo Pinda amesema, matangazo hayo yaliyosainiwa na Rais Jakaya Kikwete tangu Machi mosi, mwaka huu, yanabainisha mikoa mipya kuwa ni Geita, Katavi, Njombe na Simiyu.

Mikoa hiyo imechapishwa katika Tangazo la Serikali Namba 72.

Wilaya 19 zilizoanzishwa na kuchapishwa katika Tangazo la Serikali Namba 73 ni Buhigwe, Busega, Butiama, Chemba, Gairo, Ikungi na Itilima. Wilaya nyingine ni Kakonko, Kalambo, Kaliua, Kyerwa, Mbogwe, Mkalama na Mlele. Nyingine ni Momba, Nyang’hwale, Nyasa, Uvinza na Wanging’ombe.

Kwa mujibu wa matangazo hayo, makao makuu ya mikoa hiyo mipya minne yatakuwa kama ifuatavyo: Geita (Geita), Simiyu (Bariadi), Njombe (Njombe) na Katavi (Mpanda).

Mikoa hiyo itakuwa na wilaya zifuatazo; Geita utakuwa na wilaya tano za Bukombe, Chato, Geita, Mbongwe na Nyang’hwale; Katavi wilaya mbili za Mlele na Mpanda; Njombe utakuwa na wilaya nne za Makete, Njombe, Ludewa na Wanging’ombe wakati Simiyu utakuwa na wilaya tano za Bariadi, Busega, Maswa, Meatu na Itilima.

Makao makuu ya wilaya mpya zilizoanzishwa ni kama ifuatavyo: Buhigwe (Buhigwe); Busega (Nyashimo); Butiama (Butiama); Chemba (Chemba); Gairo (Gairo); Ikungi (Ikungi) Itilima (Lagangabilili); Kakonko (Kakonko); Kalambo (Matai) na Kaliua (Kaliua).

Nyingine ni Kyerwa (Rubwera); Mbogwe (Mbogwe); Mkalama (Nduguti); Mlele (Inyonga); Momba (Chitete); Nyang’hwale (Kharumwa); Nyasa (Mbamba Bay); Uvinza (Lugufu) na Igwachanya (Wanging’ombe).

Julai 2010, kabla Rais Kikwete hajatoa hotuba ya kulivunja Bunge, Serikali ilitoa uamuzi wa kuunda mikoa mipya minne na wilaya mpya 21.

Hata hivyo, baada ya kuhakiki mipaka ya maeneo hayo yote na kuandaa maelezo ya mipaka hiyo vizuri wilaya zilipunguzwa na kubaki 19.


source habari leo

No comments:

Post a Comment