Monday, March 5, 2012
05 MARCH.Wabunge wa Dar kumwajibisha Massaburi!
Wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam wamepanga kumwajibisha Meya wa jiji hilo, Didas Massaburi, na aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), Iddi Simba, kwa madai ya ubadhirifu wa mali kwenye shirika hilo.
Wengine watakaowajibishwa ni aliyekuwa Mkurugenzi wake, Bakari Kingobi, na wajumbe wa bodi ya shirika hilo.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Katibu wa Wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam, John Mnyika, ilieleza baada ya kikao chao, wamejipanga kuitisha kikao cha Kamati ya Fedha na Uongozi Jumatatu ijayo na mkutano maalumu wa Baraza la Madiwani wa jiji siku inayofuata.
“Kupitia mikutano hiyo tutaanza kuchukua hatua zaidi za kumwajibisha Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Massaburi, na watendaji wengine waliohusika kwa makosa ambayo tutayaeleza zaidi katika mikutano husika ya maamuzi.
“Aidha tutataka hatua za haraka zaidi za kisheria zichukuliwe kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya UDA, Iddi Simba, aliyekuwa Mkurugenzi Bakari Kingobi, wajumbe wa bodi husika na watendaji wote wa UDA waliohusika na kashfa hiyo tangu awali,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo ambayo Tanzania Daima inayo nakala yake.
Kutokana na hali ya UDA kuwa kwenye kipindi kigumu wabunge hao walieleza kuchukizwa kwa kutozingatiwa tamko lao la Agosti 4 mwaka jana ambapo waliitaka serikali kuviagiza vyombo vya dola kufanya uchunguzi.
“Tulitoa wito kwa serikali kusitisha mkataba batili na uamuzi haramu uliyofanyika wa kukabidhi hisa, mali na uendeshaji wa UDA kwa Kampuni ya Simon Group Limited ili katika kipindi hiki cha uchunguzi masuala yote ya kampuni hiyo yaratibiwe na bodi huru itayoundwa na kusimamiwa kwa mujibu wa sheria zinazohusika.
“Kamati ya wabunge wa Dar es Salaam imeazimia kuiandikia Serikali Kuu kuitaka iharakishe kuteua mjumbe wake katika bodi tajwa, ili masuala ya UDA yasimamiwe na bodi huru badala ya Simon Group kuendesha shirika hilo kama mwanahisa mkuu huku uchunguzi dhidi yake ukiendelea,” ilifafanua sehemu ya taarifa hiyo.
Wabunge hao pia wamesisitiza ni lazima mali zilizobaki za kampuni ya UDA hususani magari, majengo na viwanja kufanyiwa tathmini upya na kuunganisha mchakato wa Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (DART) ulioko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, ili kuwa na mfumo thabiti na mamlaka itakayosimamia vema mfumo wa usafiri wa umma jijini hapa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment