tuwasiliane

Monday, March 5, 2012

05 MARCH. Noah marufuku kubeba Abiria!


Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) inatarajia kusitisha leseni za usafirishaji abiria kwa kutumia gari aina ya Toyota Noah nchi nzima kuanzia Juni 31, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Meneja Leseni wa Sumatra, Leo Ngowi, watachukua
hatua hiyo kwa kuwa magari hayo ni hatari kwa usalama wa abiria na kutokana na kukosa viwango vinavyothibitiwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Ngowi alisema baada ya kuzuia leseni hizo, wanatarajia ifikapo mwakani hakutakuwa na magari hayo yanayobeba abiria.

Baadhi ya viwango ambayo magari hayo yamekosa kwa mujibu wa Ngowi ni kutokuwa na mlango wa dharura na udogo wa madirisha yake.

Alisema pia hayana uwezo wa kubeba mizigo na abiria wengi. Alisema wafanyabiashara wengi wamekuwa wakitumia magari hayo kutokana na kuwa bei nafuu kuliko magari aina ya Toyota Hiace na Toyota Costa na hivyo hukimbilia kupata faida.

Kwa mujibu wa Ngowi, Toyota Costa moja ni zaidi ya Sh milioni 50 ambayo unaweza kupata magari ya Noah mengi zaidi lakini yakiwa na ubora hafifu jambo ambalo ni hatari kwa uchumi
hususan katika sekta ya usafirishaji.

Alisema pia katika uwekezaji, magari hayo yamekuwa yakiongeza idadi ya magari mabovu
kutokana na kutohimili ubora wa barabara zilizopo nchini na wakati mwingine wafanyabiashara hushindwa kurudisha fedha zao ipasavyo.

Ngowi alisema Sumatra lazima ihakikishe abiria anatendewa haki katika kulipa nauli na mwenye Noah hawezi kutoza nauli iliyopangwa na Sumatra kwa kuwa akifuata nauli hizo, hatarudisha gharama zake.

“Unajua gari hizi zinabeba abiria saba na zaidi kidogo, sasa ni lazima apandishe nauli zaidi ya ilivyopangwa jambo ambalo linamuumiza abiria, nawaomba wafanyabiashara kununua magari
yanayokidhi viwango hata kama ni ya gharama,” alisisitiza Ngowi.

Alisema japokuwa sheria inaruhusu kutolewa kwa leseni kwa gari lenye uwezo wa kubeba abiria zaidi ya saba, lakini wafanyabiashara hao hubeba abiria nane na zaidi pamoja na mizigo na kuweka usalama kwa abiria hatarini.

Ngowi alisema kutokana na kutokuwa salama, kumekuwa na ajali nyingi za magari hayo yanayobeba abiria na kusababisha madhara makubwa tofauti na magari mengine ambayo ni imara.

“Kutokana na hali hiyo, kuanzia Julai hatutatoa kabisa leseni mpya nchi nzima kwa wasafirishaji wa magari ya Noah na kwa wale walizonazo sasa zikiisha hawatawapatiwa tena ili
kufikia malengo ya kudhibiti usafiri huo hatari,” alisisitiza Ngowi.

No comments:

Post a Comment