Wednesday, February 29, 2012
29 FEB.STARS VS MAMBAZ LEO UWANJA WA TAIFA
TIMU ya soka ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ leo inaanza kampeni zake za kuwania kufuzu fainali za Afrika mwakani itakapocheza na Msumbiji ‘Mambas’ Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mechi hiyo ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kwa ajili ya kufuzu fainali za Kombe la Shirikisho hilo kwa Mataifa ya Afrika (Afcon) ambazo zitafanyika mwakani nchini Afrika
Kusini.
Taifa Stars haijafuzu fainali hizo tangu ilipocheza kwa mara ya kwanza mwaka 1980, wakati fainali hizo zilipofanyika Lagos, Nigeria, wakati huo fainali hizo zikishirikisha timu nane tu
tofauti na 16 za sasa.
Mchezo wa leo Stars inakutana na Msumbiji ambayo katika mechi ya mwisho ya mashindano zilipocheza Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam mwaka 2007 Stars ililala bao 1-0 lililofungwa na Tico Tico.
Lakini pia Msumbiji iliifunga Stars mabao 2-0 mwaka jana katika mechi ya kirafiki ya kimataifa ya kufungua Uwanja mpya wa Zimpeto.
Taifa Stars inaingia uwanjani ikiwa imepata mechi moja ya kujipima nguvu dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) iliyofanyika Alhamisi iliyopita na timu hizo kutofungana.
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Jan Poulsen alisema jana kuwa vijana wake wamejiandaa vizuri, hivyo kuwaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi kuwaunga mkono.
“Naifahamu Msumbiji ni timu nzuri, tunajipanga iwezekanavyo kuhakikisha tunawapa raha Watanzania, nakumbuka mechi ya mwisho tulifungwa mabao 2-0, lakini tumejiandaa
kuwakabili.
“Naomba Watanzania tuuchukulie umuhimu mchezo huu, waje watushangilie,” alisema Poulsen.
Naye Kocha Mkuu wa Mambas, Gert Engels, alisema wanauchukulia uzito mkubwa mchezo huo na kwamba ushindi wa leo utakuwa wa umuhimu mkubwa kwao.
Taifa Stars leo itawategemea zaidi washambuliaji wake Abdi Kassim, John Bocco na Mrisho Ngasa, huku safu ya kiungo ikiwa na Nizar Khalfan na Shaaban Nditi, wakati kwenye
ulinzi ni Aggey Morris na Juma Nyosso ambao wanatakiwa kuhakikisha kipa Juma Kaseja hapati madhara.
Karibu wiki moja iliyopita kulifanyika mchezo wa fainali ya Afcon kati ya Zambia na Ivory Coast iliyofanyika nchini Gabon, ambapo nchi hiyo na Equatorial Guinea ziliandaa fainali za mwaka huu kwa ubia. Zambia iliibuka bingwa wa mashindano hayo.
Fainali hizo zinafuatana kutokana na uamuzi uliofanywa na Caf, ambapo lengo lake la kuandaa fainali nyingine za Afcon mwakani ni kutaka zipishane na zile za Kombe la Dunia inazoandaliwa
na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (Fifa), ambazo hufanyika kila baada ya miaka minne.
Baada ya Afcon ya mwakani itafanyika tena mwaka 2015.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment