Wednesday, February 29, 2012
29 FEB. Yanga kwenda Misri kesho
KIKOSI cha wachezaji 20 wa Yanga kinaondoka kesho na ndege ya Shirika la Egypt Air kuelekea jijini Cairo, Misri kwa mchezo wao wa marudiano wa kuwania ubingwa wa klabu bingwa Afrika dhidi ya Zamalek utakaofanyika kwenye Uwanja wa Jeshi nchini humo.
Yanga ambayo ilikubali sare ya bao 1-1 nyumbani itarudiana Machi 3 na Zamalek na inaondokam kesho na matumaini mengi huku ikiahidi kufanya vyema na kufanikiwa kusonga mbele katika michuano hiyo mikubwa barani Afrika.
Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu akiongea na waandishi wa habari jana alisema kuwa mara baada ya mchezo wa leo wa timu ya Taifa dhidi ya Msumbuji kocha mkuu Kostadin Papic anatarajia kutangaza majina ya wachezaji 20 watakaoondoka siku inayofuata tayari kwa mchezo huo.
Alisema mbali na kikosi hicho pia safari yao itajumuhisha mashabiki 10 tu watakaoongozana na timu kwa ajili ya kuihamasisha timu yao mara baada ya Shirikisho la soka Afrika CAF kutoruhusu mashabiki kuhudhuria katika mchezo huo tangu ilipotokea vurugu katika moja ya mechi za Ligi Kuu ya Misri na kusababisha mashabiki mashabiki 74 nchini humo kufariki dunia.
"Kwa kiasi kikubwa maandalizi yanakwenda vizuri na hivi sasa tupo katika matayarisho ya mwisho huku tukisubiri mchezo wa leo (kesho) wa Stars ili kocha aweze kutangaza wachezaji watakaoondoka tayari kwa pambano letu la marudiano,"alisema Sendeu.
Aidha aliongeza kuwa mshambuliaji wao Haruna Niyonzima ambaye yupo nchini kwake akiitumikia timu ya Taifa lake atatumiwa tiketi ya moja kwa moja na ataungana na wenzake nchini Misri endapo jitihada za kuongozana nao zitashindikana kwa hapa nyumbani.
Yanga inahitaji ushindi ugenini mara baada ya kukubali sare ya 1-1 nyumbani ili iweze kusonga mbele katika michuano hiyo ya klabu bingwa Afrika.WAKATI HUOHUO
KIUNGO Rashid Gumbo na kipa Yaw Berko ni miongoni mwa wachezaji saba walioachwa kwenye kikosi cha Yanga kwa ajili ya mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Soka Afrika dhidi ya Zamalek ya Misri itakayofanyika Machi 3, mjini Cairo, Misri.
Kwa siku za hivi karibuni, Gumbo aliingia kwenye malumbano na kocha wa Kostadin Papic. Baadaye Papic alitoa taarifa kwamba Gumbo asingecheza mechi ya kwanza na ile ya marudiano kwa sababu alikuwa majeruhi.Hata hivyo mchezaji huyo alipinga taarifa hizo kwamba alikuwa anaumwa na kusema kulikuwa na jambo linafichwa kuhusu yeye.
Kabla ya taarifa hiyo, Papic pia aliwahi kuzungumza kwamba jina la mchezaji huyo halikuwa miongoni mwa yale yalipelekwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Gumbo alicheza Kombe la Mapinduzi Januari mwaka huu baada ya kuitwa katika kikosi cha pili ambacho kilitolewa katika hatua ya awali kufuatia kufungwa na Azam FC.
Akiongea jana, Gumbo alisema alijua asingesafiri kwenda Misri. "Nilifahamu mapema kwamba siwezi kuwa miongoni mwa wachezaji watakaokwenda Misri," alisema Gumbo kwa masikitiko.
“Siwezi kusema kwamba nina matatizo na kocha, lakini mazingira yanaonyesha kila kitu ingawa niko tayari kuendelea kuitumikia timu yangu vizuro kwenye mechi za Ligi Kuu na michuano ya kimataifa kama nilivyofanya kwenye michuano ya Kombe la Kagame," alisema Gumbo.Kwa upande wa kipa Yaw Berko yeye ameachwa kwa sababu ya kuwa mgonjwa, sambamba na mchezaji Salum Telela.
Wengine walioachwa ni Zuberi Ubwa, Idrissa Rashid, Godfrey Bonny na Mohamed Mbegu.Wanaosafiri na timu ni pamoja na Shaaban Kado, Said Mohamed, Shadrack Nsajigwa, Godfrey Taita, Stephano Mwasika, Oscar Joshua, Abuu Ubwa, Nadir”Cannavaro” Haroub na Athuman Chuji” Idd.
Wengine ni Juma Seif Kijiko, Nurdin Bakari, Omega Seme, Ibrahim Job, Shamte Ali, Haruna Niyonzima, Keneth Asamoah, Davies Mwape, Jerryson Tegete, Pius Kisambale na Hamis Kiiza.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment